110 wanaswa kwa uhalifu, ‘unga’ Dar
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu 110 kwa makosa mbalimbali ya kihalifu pamoja na dawa za kulevya kwa siku tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema watu hao wamekamatwa kutokana na msako na operesheni kali, inayoendeshwa na jeshi hilo ya kuwakamata wahalifu wa makosa mbalimbali.
Kamanda Sirro alisema makosa hayo ni kupatikana na dawa za kulevya, unyang’anyi wa kutumia silaha, utapeli, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari, kuuza pombe haramu ya gongo.
Alisema katika operesheni hiyo ambayo ni endelevu, kete 102 za dawa za kulevya zilikamatwa, puli 95, misokoto ya bhangi 106 na pombe haramu ya gongo lita 10.
“Operesheni hii kali ya kuwashika wahalifu wa makosa mbalimbali ikiwemo kupatikana dawa za kulevya ni endelevu hivyo raia wema wanaombwa kuendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa jeshi la polisi ili kurahisisha kukamatwa kwa wahalifu hao na hatua kali za kisheria zifuate dhidi yao,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema watuhumiwa wote, wanaendelea kuhojiwa kulingana na makosa yao na upelelezi utakapokamilika, watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.
Katika tukio jingine, jeshi hilo limemkamata mmiliki wa wa duka la kuuza vileo vya jumla na rejareja akiwa na katoni 175 za pombe ya viroba.
Alitaja pombe alizokamatwa nazo katika duka lake ni katoni 17za Boss nanasi, katoni nane za Kiroba original, Konyagi katoni 60, Zanzi katoni 10, Valeur 20 zilizokutwa nyumbani kwake baada ya upekuzi.
Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro amesema wamekamata majambazi wawili na silaha moja aina ya Bereta baada ya majibizano ya risasi kati ya polisi na majambazi.
Alisema tukio hilo ni la Machi 12, mwaka huu maeneo ya Vijibweni katika Manispaa ya Kigamboni, ambako waliwakamata watu hao wenye umri kati ya miaka 25 hadi 30 wakiwa na bastola moja aina ya Bereta ikiwa na risasi ndani ya magazini.
Alisema kabla ya tukio hilo, jeshi lilipokea taarifa za uwepo wa majambazi watatu ambao walipanga kufanya tukio la uhalifu katika eneo hilo, ndipo askari waliweka mtego na kufanikiwa kuwakamata baada ya majibizano ya risasi ambapo majambazi hao walijeruhiwa vibaya.
Credit: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment