METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 15, 2017

11 wafanyiwa upasuaji Taasisi ya Moyo ya Kikwete

WAGONJWA 11 wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo, inayofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ushirikiano na madaktari wenzao wa Taasisi ya Open Heart International ya Australia.

Taarifa iliyotolewa na JKCI, ilimkariri Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo, Dk Bashir Nyangasa wakati akielezea jinsi kambi hiyo ya upasuaji inavyoendelea kutoa matibabu kwa wagonjwa.

Dk Nyangasa alisema, “Kwa kushirikiana na washirika wetu wa OHI tulianza kambi maalum ya upasuaji kuanzia tarehe kumi mwezi huu wa tatu hadi leo tarehe kumi na nne (jana), tumefanya upasuaji kwa wagonjwa kumi na moja ambao wanaendelea vizuri. Kati ya hao watoto ni tisa na watu wazima ni wawili.”

Alisema katika kambi hiyo ambayo inamalizika Machi 17, mwaka huu, walipanga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 25 kati ya hao watoto ni 15 na watu wazima ni 10.

Kuhusu mahitaji ya damu kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo, Dk Nyangasa alisema wagonjwa hao wanahitaji damu nyingi, hivyo aliwaomba wananchi wajitokeze kuchangia damu, ambayo itatumika kwa wagonjwa.

“Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu na uchangiaji huu wa damu usifanyike mara moja bali uwe endelevu kwani Taasisi inatoa huduma kwa wagonjwa wakati wote siyo wakati wa kambi maalum za matibabu ya moyo pekee yake,” alisisitiza Dk Nyangasa.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, JKCI kwa kushirikiana na baadhi ya washirika wake wa nje ya nchi ambao ni Madaktari Afrika wa Marekani, Hospitali za Apollo, Bangalore na BLK zote za India na Open Heart International ya Australia, wamefanya matibabu ya moyo ya kufungua na bila kufungua kifua kwa wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika taasisi hiyo.

Credit: Habari Leo
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com