METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 15, 2017

Watumishi 2,000 wahamia Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama

AWAMU ya kwanza ya serikali kuhamia Dodoma imekamilika kwa watumishi wa wizara zaidi ya 2,059 kuingia mjini hapa, huku Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiongoza kwa kuwa na watumishi wengi.

Kuongezeka kwa wafanyakazi hao, kunaufanya Mkoa wa Dodoma uwe na wakazi zaidi ya 2,085,647.

Akizungumza na gazeti hili, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema uhamisho huo umefanyika vizuri.

“Katika awamu hii ya uhamisho inahusisha mawaziri, naibu mawaziri, makatibu, naibu makatibu na baadhi ya wakurugenzi wa wizara,” alieleza Jenista.

Katika orodha hiyo, Ofisi ya Rais Ikulu haimo, lakini na Ofisi ya Rais Tamisemi ilikuwapo mkoani Dodoma siku nyingi.

Katika kuitikia mwito wa Rais John Magufuli kuhamia Dodoma, wizara ambayo watumishi wengi wamehamia ni Ardhí ambayo wamehamia watumishi 364.

Wizara nyingine ni Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (313), Kilimo, Mifugo na Uvuvi (218), Fedha na Mipango (184), Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (132) na Ofisi ya Waziri Mkuu (116).

Wizara ya Maji na Umwagiliaji zimegongana na ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kila moja kuhamisha watumishi wa wizara 104 kila moja.

Wizara zilizohamisha pungufu ya watumishi 100 ni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umama na Utawala Bora (78), Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi (66), Maliasili na Utalii (55); wakati zilizohamisha watumishi pungufu ya 50 ni Nishati na Madini (47), sawa na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (47), Mambo ya Ndani ya Nchi (44), Ofisi ya Makamu wa Rais (44) na Katiba na Sheria (43).

Nyingine ni Viwanda, Biashara na Uwekezaji (42), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (33) na Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (25) ambayo imehamisha wafanyakazi wachache zaidi.

Awamu ya pili ya kuhamia Dodoma ilianza tangu Machi mosi na itakwenda hadi mwisho wa Agosti ambapo wafanyakazi wengi watahamia zaidi.

Dodoma ni mji wa Tanzania ya kati na ulitangazwa kuwa mji mkuu wa Tanzania mwaka 1973, utekelezaji wake umefanyika mwaka 2017.

Mkoa wa Dodoma una eneo la kilometa za mraba 41,311 na idadi ya watu milioni 2.1 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

Kati yao, wanaume ni 1,014,974 na wanawake 1,068,614. Kaya zilizopo ni 453,844 ambazo zina wastani ya watu 4.6 kwa kila moja.

Credit: Habari leo
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com