Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa
atakayepokea rushwa kutoka kwa wauzaji, wasambazaji na watumiaji wa
Madawa ya Kulevya.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam
wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha Baraza la Taifa la kudhibiti
dawa za kulevya nchini.
“Sheria ya udhibiti wa madawa ya kulevya
itumike vizuri, Serikali na Baraza halitahitaji mtu yeyote mwenye
mamlaka kupokea rushwa ikigundulika hatua kali zitachukuliwa” alifafanua
Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano imedhamiria kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya
udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini ambayo yamekuwa yakifanywa na
Serikali za Awamu zilizotangulia.
Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa
mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ni vita inayotakiwa kupigana kwa
nguvu kubwa kwani madhara ya dawa hizo ni kubwa kwa jamii hususani
vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.
“Tunahitaji ushirikiano wa karibu wa
pande zote mbili za Muungano kwani tatizo hili limeathiri pande zote na
ukanda wa bahari unatumika sana kama njia ya kuingiza dawa hizo”
“Wakuu wa Mikoa mna kazi kubwa katika
vita hii, mkiwa wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama mpo kwenye
nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Taratibu zilizopo” alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo Waziri Mkuu alibainisha kuwa,
wajibu wa Baraza ni kusimamia utekelezaji wa Sera ya Udhibiti wa Dawa
za Kulevya nchini, ambapo jukumu hilo ni kubwa na wajumbe wa Baraza hilo
wanatakiwa kulitekeleza kwa uadilifu na umahiri mkubwa.
Baraza la Taifa la kudhibiti Dawa za
Kulevya limeanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 ambapo Waziri Mkuu
ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo pamoja na wajumbe wengine wakiwemo
Waziri anayeshughulikia Mambo ya Sheria, Waziri anayeshughulikia Mambo
ya Ndani ya Nchi.
Wengine ni Waziri anayeshughulikia Afya,
waziri anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Waziri anayeshughulikia
Mambo ya Nchi za Nje, Waziri anayeshughulikia Fedha, Waziri
anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Waziri anayeshughulikia Elimu,
Waziri anayeshughulikia Kilimo, Waziri anayeshughulikia Uchukuzi na
Waziri anayeshughulikia Ulinzi.
0 comments:
Post a Comment