METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, February 14, 2017

RC MTAKA: UFAULU MZURI WA WANAFUNZI UPO MIKONONI MWA WALIMU

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka akisisitiza jambo wakati wa kikao na walimu wa shule za Umma na Binafsi wa madarasa ambayo yanataraji kufanya mtihani mwaka huu wa 2017
Walimu wa shule za Umma na Binafsi wa madarasa ambayo yanataraji kufanya mtihani mwaka huu wa 2017 wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka

Afisa elimu wa Mkoa wa Simiyu Ndg Julius Nestory akielezea hali ya ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne kwa kipindi cha miaka mitano
 Rc Mtaka alipokuwa akisaini kitabu cha wageni
 Walimu wakiwa makini kumsikiliza Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka (katikati),akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho kulia kwake ni Afisa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mji Ndg Alex Rwabigene na kushoto kwake ni Afisa elimu wa Mkoa wa Simiyu Ndg Julius Nestory
Afisa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mji Ndg Alex Rwabigene akizitaja changamoto zinazoikabili sekta ya elimu
 Walimu wakisikiliza kwa makini
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa sekta ya elimu Mkoani humo


Na Mathias Canal, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka amesema kuwa Matokeo ya ufaulu ulio bora na wa kiwango cha juu upo mikononi mwa wazazi/walezi,na Jamii lakini zaidi ni kwa walimu ambao utaalamu wao umejikita katika kumkwamua mwanafunzi kutoka daraja sirufi hadi kufikia daraja la kwanza.

Mhe Mtaka amebainisha hayo wakati wa kikao chake na walimu wa shule za Umma na Binafsi wa madarasa ambayo yanataraji kufanya mtihani mwaka huu wa 2017 kilichofanyika katika Ukumbi wa shule ya Sekondari Bariadi huku akiwasisitiza walimu kutumia weledi wao zaidi kuitumikia jamii na kuimarisha kiwango cha ufaulu katika Mkoa huo.

Kikao hicho kilichokuwa na lengo la kukubaliana na kupata namna bora ya kuboresha elimu na kiwango cha ufaulu Mkoani Simiyu, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwepo kwa kambi maalumu kwa ajili ya wanafunzi kufundishwa kwani mafanikio ya jitihada zao pekee katika kujisomea na kufundishwa darasani haitoshi bali wanahitaji kuongezewa msukumo na utaalamu zaidi kwa masomo ya ziada.

“Kama katika Mkoa wetu na Tanzania kwa ujumla mara nyingi huwa kuna kambi mbalimbali za michezo zinazoanzia ngazi za chini kabisa hadi kambi za ngazi za kitaifa ambazo zinafanikiwa vizuri kwanini tusiwe na kambi maalumu kwa ajili ya nyongeza ya masomo” 

“Sote hapa kwa umoja wetu ni lazima tutambue kuwa matokeo bora ya wanafunzi waliopo darasa la saba, wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita yapo mikononi mwa walimu hivyo njia bora ni kutatua matatizo yanayowakabili walimu ili tuweze kufikia lengo” Alisisitiza Mhe Mtaka

RC Mtaka alisema kuwa walimu Mkoani Simiyu wana kazi kubwa kuliko hata walimu waliopo katika Mikoa mingine kwani wanatakiwa kuwabadilisha wanafunzi kutoka katika mtazamo wa mila zao na kuhamia katika muktadha wa elimu jambo ambalo katika maeneo mengine sio kubwa sana.

Saambamba na hayo pia amewataka viongozi wote katika kada mbalimbali kutumia vyema uongozi wao kwa kuwatumikia wananchi huku akiwasihi kutumia lugha nzuri pindi wanapozungumza nao kwani kiongozi yeyote atakayetumia lugha mbaya anapaswa kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.

Akisoma taarifa ya ya awali kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa, Afisa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mji Ndg Alex Rwabigene amezitaja changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kuwa ni pamoja na Upungufu wa vitabu vya kiada na ziada kwa masomo ya sanaa, Umbali wa kutoka nyumbani hadi shuleni kwa baadhi ya shule za Sekondari hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kushinda njaa na wengine kuangukia kwenye mikono ya watu wabaya hasa kwa wanafunzi wa kike, na Upungufu wa watumishi wenye sifa katika ngazi ya kata wenye uwezo wa kutekeleza majukumu ya idara ya elimu.

Hata hivyo ameeleza kuwa tayari kuna mikakati ya kuinua taaluma katika shule za sekondari kuwa ni pamoja na kuanzisha mitihani na mazoezi ya kila siku asubuhi kabla ya ratiba ya kawaida ya siku kwa madarasa ya mitihani yaani kidato cha pili, nne na cha sita, Kusimamia zoezi la utoaji chakula shuleni, Kuchangia upatikanaji wa chakula kupitia shule kwa kulima mazao, Kutofunga shule kwa wanafunzi wa madarasa yenye mitihani wakati wa likizo ya mwezi wa sita, Kufanya ukaguzi wa ufuatiliaji wa taaluma mara kwa mara, na Afisa elimu kwa kushirikiana na Waratibu wa elimu kata kufatilia walimu wasiowajibika na kuchukuliwa hatua.

Naye afisa elimu wa Mkoa wa Simiyu Ndg Julius Nestory alisema kuwa hali ya ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2012 mpaka mwaka 2017 kiwango cha ufaulu kimekuwa kikiongezeka tangu mwaka 2013 hadi 2016 ambapo ufaulu uliongezeka kwa asilimia 64.87% mwaka 2013, asilimia 73.40% mwaka 2014, Asilimia 73.61% mwaka 2015, na asilimia 74.30% mwaka 2016.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com