METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, February 14, 2017

RC MTAKA ASEMA HAKUNA STAILI RASMI YA KUPAMBANA NA ADUI UWAPO VITANI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka akisistiza jambo wakati akizungumza na wasanii wa Dansi walipomtembelea ofisini kwake
 Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya uchapishaji wa Magazeti ya serikali (TSN) Tanzania Standard Newspaper Dkt Jim Yonazi alipokuwa akizungumza na wasanii hao
Rc Mtaka akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa wasanii kuhusu namna wanavyofahamu kadhia ya Dawa za kulevya



Na Mathias Canal, Simiyu

Imebainika kuwa katika kupambana na kadhia mbalimbali nchini ikiwemo kutokomeza Dawa za Kulevya staili yoyote inaweza kutumika ili kuwabaini watumiaji, wauzaji na wasafirishaji wa Dawa za Kulevya na hatimaye kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka wakati akizungumza na wasanii mbalimbali wa muziki wa Dansi waliozuru ofisini kwake ambapo amewasihi wasanii hao kuunga mkono juhudi za serikali za kupinga mihadarati nchini kwa kutunga wimbo maalumu.

Rc Mtaka amewapongeza wasanii hao kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuitangaza Tanzania kunako nchi za nje na kutangaza lugha ya Taifa ya Kiswahili pindi wanapokuwa majukwaani kutumbuiza huku mashabiki wakiwaunga mkono kwa kuzikariri na kuziimba nyimbo zao.

Amewasihi watanzania kutofanya kazi kwa woga kwa sababu ya kuogopa watu watawasema vibaya ama kuwatukana kwa sababu ya bidii na nidhamu katika utendaji.

Rc Mtaka amesema kuwa kile kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda kwa kuwataja hadharani watumiaji na wauzaji wa mihadarati nchini kuwa ni kitendo cha ujasiri wa hali ya juu kwani kila jambo lazima liwe na mwanzo wake na muendelezo katika nchi.

Hata hivyo amewasihi wasanii hao kutojihusisha na matumizi na usafirishaji wa Dawa za Kulevya kwani katika kipindi kirefu wamekuwa wakituhumiwa kutumika katika usafirishaji wa mihadarati.
Amewasihi wasanii hao kujenga mfumo mzuri wa kuwasaidia wasanii wengine ambapo alipendekeza wasanii hao kukutana na kuanzisha baraza la washauri ili kukemea matumizi ya Dawa za kulevya.

Kwa upande wake Msanii wa mziki wa Dansi nchini Ally Choki akizungumza kwa niaba ya wasanii wenzake amesema kuwa Asilimia kubwa ya watanzania wanavuta makapi ya unga ndio maana wamekuwa wakiathirika na hatimaye wanafariki dunia.

Amesema kuwa kampeni hiyo ya kupambana na Matumizi ya Dawa za kulevya nchini itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwasaidia watanzania walioathirika na matumizi ya Dawa hizo kuachana nazo na kuimarika kwa afya zao na kuokoa kizazi kikubwa nchini.

Hata hivyo Ally Choki amemueleza Mkuu huyo wa Mkoa dhamira yake ya kuwania Ubunge katika Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoani Pwani kupitia tiketi ya Chama Cha Mpanduzi (CCM) hivyo ameomba kumunga mkono wakati utakapowadia.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com