Mwanamke
mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Mama Saidi’ anashikiliwa na polisi kwa
tuhuma za kumuwekea pilipili kwenye macho mtoto wake wa kambo anayesoma
darasa la sita kwa madai ya kutofua nguo za shule.
Tukio
hilo limetokea Mtaa wa Tabata Magharibi na kuripotiwa kwenye ofisi ya
Serikali ya Mtaa huo juzi, kabla ya mwanamke huyo kukamatwa na kupelekwa
Kituo cha Polisi Tabata ambapo anashikiliwa hadi sasa.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala,
Salum Amaduni alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema upelelezi
bado unaendelea.
“Mtuhumiwa
atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika, ikiwa ni pamoja
na kupokea taarifa ya daktari ambayo itaonyesha ni kwa kiasi gani mtoto
huyo ameumia au madhara aliyoyapata kutokana na kitendo kile,” alisema Amaduni na kuongeza:
“Bado tunakusanya ushahidi, ukikamilika tutapeleka jalada kwa mwanasheria wa Serikali kwa hatua za mashtaka.”
Awali
majirani walidai imekuwa kawaida kwa mwanamke huyo kumnyanyasa mtoto
huyo wa kambo, lakini Kamanda Amaduni alisema tukio hilo ni la kwanza
kuripotiwa kutoka kwa mwanamke huyo na si kama wanavyoeleza majirani
zake.
Mtendaji
wa mtaa huo, Hamza Ramadhani alisema mtoto huyo alipofikishwa ofisini
kwake alikuwa haoni kutokana na athari za pilipili, ndipo alipopelekwa
Kituo cha Afya Tabata.
“Lakini
walipomuangalia waliamua kumpeleka Hospitali ya Amana na taarifa
nilizanazo kwa sasa jana(juzi) amesharuhusiwa yupo nyumbani na mwenzake
ila mama ndio bado yupo polisi,” alisema.
Jirani
wa mtoto huyo, Gowely Anthoy alisema kwa kipindi kirefu kulikuwa na
viashiria vya mtoto huyo kunyanyaswa lakini hakuna aliyeweza kuhoji.
“Mtoto
mwenyewe amekuwa akisema tangu siku nyingi mama hamhudumii ipasavyo,
lakini tulikuwa tukichukulia kama masuala ya kawaida ya watoto, lakini
sasa tumejua ni kweli,” alisema.
0 comments:
Post a Comment