METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, February 7, 2017

MABUSHA, MATENDE NA USUBI BADO NI TATIZO MUFINDI


Halmshauri ya Wilaya ya Mufindi, italazimika kurudia zoezi la utoaji kinga tiba kwa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele baada ya utafiti wa kitabibu kutoka wizara ya afya kubaini uwepo wa vimelea vya magonjwa hayo kwa asilimia kubwa ya wakazi wa halmashauri hiyo.

Taarifa ya idara ya afya kupitia Afisa habari na mawasiliano wa halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bw. Ndimmyake Mwakapiso , imeyataja magojwa hayo manne kuwa ni Ugonjwa wa Mabusha na Matende, Mivyoo ya tumbo sanjari na ugonjwa wa usubi ambao huathiri macho ya binadamu kwa kusababisha upofu.

Amesema baada ya kukamilika kwa zoezi la utoaji kinga tiba mapema mwaka jana, ni kawaida kwa wizara ya afya kuendesha utafiti kwa lengo kutadhimini na kujiridhisha kama kinga tiba iliyotolewa imekidhi matarajio au la, na ndipo ilipogundulika kuwa bado kunavimelea vya maabukizi ya magonjwa hayo miongoni mwa jamii ndani ya halmashauri hiyo.

Mwakapiso, ameongeza kuwa kinga tiba hiyo itatolewa na watoa huduma waliopo katika ngazi ya jamii husika ambao wamepata mafunzo maalum na kujengewa uwezo wa kutekeleza jukumu hilo kwa weledi mkubwa, zoezi ambalo litaendeshwa kuanzia jumatatu ya tarehe 06 mwezi huu na litadumu kwa muda wa siku 06 pekee.

Aidha, ametoa rai kwa wakazi wote wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watoa huduma watakaofika katika kaya kuwapatia kinga tiba hiyo muhimu kwa ustawi wa afya zao na maendeleo ya taifa, kwa kuzingatia kuwa afya njema ndio chimbuko la maendeleo ya familia na taifa lolote duani.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com