Na
Zuena Msuya, Pwani,
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini inaangalia namna bora ya
kuimarisha soko la chumvi inayozalishwa nchini yenye uwezo wa kukidhi mahitaji
ya ndani na ziada, kwa kuzuia ile inayoingizwa kutoka nchi za nje.
Nyongo alisema hayo, wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani, Julai 23, 2018, baada ya kutembelea Mgodi wa kuzalisha chumvi wa kampuni
ya Stanley and Sons ulioanzishwa mwaka 1948/49 uliopo katika Kijiji cha Kitame
wilayani humo.
Akizungumzia uzalishaji chumvi, Nyongo
alitolea mfano mgodi pekee wa Stanley kuwa, huzalisha chumvi kati ya tani 4000
hadi 6000 kwa mwaka kulingana na hali ya hewa, licha ya kuwepo migodi mingi ya
uzalishaji chumvi katika baadhi ya Mikoa nchini ambapo mara nyingi wazalishaji wamekuwa
wakilalamikia ukosefu wa soko la chumvi wanayozalisha.
Alitaja baadhi ya Mikoa iliyokuwa na
migodi ya kuchimba na kuzalisha chumvi kuwa ni pamoja Pwani yenye zaidi ya mgozi
mmoja, Kigoma katika eneo la Uvinza, Lindi pamoja na Mtwara.
" Tanzania ina migodi mingi ya
kuchimba na kuzalisha chumvi bora, ya kutosha na yenye kukidhi mahitaji ya
ndani na kuuza nje, hivyo ni wakati sasa, serikali kuangalia namna bora ya
kulinda soko la ndani la chumvi kwa kuzuia ile inayoingizwa kutoka nje, ili
wazalishaji waweze kupata soko la uhakika", alisisitiza Nyongo.
Aidha aliwaagiza wachimbaji na
wazalishaji wa chumvi nchi, kusindika chumvi hiyo katika ubora unaotakiwa na
kukidhi viwango vya soko la Kimataifa kwa kuzingatia kuwa, Tanzania inazalisha
chumvi iliyobora.
Sambamba na hilo, alieleza kuwa
kwakuwa chumvi ni bidhaa mtambuka inayotumika kama chakula, dawa, pamoja na
kuwa ni madini hivyo, aliwataka wachimbaji na wazalishaji wa chumvi, kusindika
chumvi hiyo katika ujazo tofauti na kwa bei nafuu ili kila mmoja aweze kumudu
gharama za kununua chumvi hiyo kwa matumizi husika ikiwemo majumbani, viwandani
na hata katika mifugo.
Pia, alisema wazalishaji wakubwa wawasaidie
na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wa chumvi ili na wao waweze kuuza na
kusambaza chumvi hiyo ili iwafikie watumiaji wa aina mbalimbali kwa urahisi
zaidi na kukidhi mahitaji ya walaji kwa wakati.
" Watumiaji wengi wa chumvi
majumbani wananunua na kutumia iliyosindikwa katika ile mifuko midogo ya robo
au nusu kilo, sasa ninyi wachimbaji na wazalishaji wa chumvi muangalie namna ya
kuwafikia watumiaji wote wa chumvi hapa nchini, hii italeta tija kwa watanzania
kutangaza na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini", alisema Nyongo.
Nyongo aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali
inaendelea kuunga mkono juhudi za wachimbaji na wazalishaji wa chumvi nchini
kwa kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha kufanya kazi hiyo katika kiwango
kikubwa na ubora unaotakiwa.
Pamoja na mambo mengine, alisema kuwa,
tayari serikali imewafutia wachimbaji na wazalishaji chumvi, kodi kumi na moja
ambazo zilikuwa kero kubwa kwao, na kwamba serikali inaendelea kushughulikia
vikwazo vingine vinavyokwamisha shughuli zao.
Aidha alitaja baadhi ya nchi
zinazonunua chumvi ya Tanzania kuwa ni pamoja na Jamuhuri ya Watu Congo,
Malawi, Msumbiji,pamoja na Uganda na kusema kuwa lengo ni kufikia nchi nyingi
zaidi duniani.
Aliwaagiza wachimbaji na wazalishaji
wote wa chumvi nchini kulipa mirabaha na tozo mbalimbali na kushiki katika
shughuli za kijamii zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini, kwa lengo la
kuongeza pato la taifa kwa manufaa ya watanzania.
Mmoja wa Wakurugenzi katika Mgodi wa Chumvi
wa Kampuni ya Stanley and Sons, Richard Stanley aliiomba serikali kuboresha miundombinu
ya barabara itakayorahisisha usafirishaji ya chumvi hiyo, kwa kuwa katika
kipindi cha wa mvua hakuna vyombo vya usafiri vinavyoweza kufika katika eneo
hilo.
Vilevile, Richard aliiomba serikali
kuwapelekea huduma ya umeme katika kijiji hicho ili kupunguza gharama za
uzalishaji ambapo kwa sasa hutumia mafuta mazito kuendeshea mashine za
uzalishaji.
Hata hivyo, Naibu Waziri Nyongo
aliwahakikisha wawekezaji hao kuwa changamoto zote zitashughulikiwa katika
kipindi kifupi kijacho kwa kuwa nia ya serikali ni kuwawezesha wawekezaji wa
ndani na nje waweze kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri na rafiki ili
kuunga mkono azma ya serikali ya kuwa tanzania ya viwanda kutokana na
rasilimali zilizopo nchini.
Captions
picha
1
Naibu Waziri Stanslaus
Nyongo,( katikati) wakijadiliana hatua za uzalishaji chumvi, katika mgodi wa
chumvi wa kampuni ya Stanley and Sons, wa pili kushoro ni mmoja wa Wakurugenzi wa
mgodi huo, Richard Stanley.
picha
2
Naibu Waziri, Stanslaus
Nyongo,(kulia) akiingia katika moja ya vitalu vya mgodi wa chumvi wa kampuni ya
Stanley and Sons.
Picha 3
Moja ya mashine za kuvuna chumvi katika mgodi wa kampuni ya Stanley
and Sons.
Picha
4
Naibu Waziri Stanslaus
Nyongo( aliyeinama) akigusa chumvi iliyorundikwa tayari kwa kufungashwa katika
mifuko kwa ajili ya kuuzwa kwa watumiaji.
Picha
5
Baadhi ya vitalu vya kuzalisha chumvi katika mgodi wa kampuni ya
Stanley and Son, uliopo katika Kijiji cha Kitame wilayani Bagamoyo mkoani
Pwani.
0 comments:
Post a Comment