WAZIRI
wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wajumbe
wa Kamati ya Kimataifa inayojishughulisha na kuzuia mauaji ya kimbari
katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu, kuangalia upya mikakati ya
kuondoa vitendo vya mauaji ya kimbari na ukiukwaji wa haki za binadamu
katika ukanda huo.
Amesema Ukanda wa Maziwa Makuu umekuwa
ukishuhudia vitendo vya mauaji ya kimbari vikishamiri licha ya kwamba
kila nchi imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali na kusaini makubaliano
ya kikanda na kimataifa ya kuzuia vitendo hivyo.
Alisema wakati umefika wa kujiangalia
ni kwa nini vitendo hivyo vimekuwa vikishamiri pamoja na jitihada zote
ambazo kila nchi imekuwa ikizichukua ili kukomesha vitendo hivyo.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo wakati
akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo na kubadilisha uzoefu
na wajumbe wa kamati hiyo kwa nchi za Maziwa Makuu yanayofanyika jijini
Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yanajumuisha wajumbe
kutoka nchi za Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan Kusini na wenyeji Tanzania.
“Ni wazi kuwa siku hizi mwelekeo wa
matukio ya kihalifu umebadilika, zimeibuka njia nyingi mpya
zinazosababisha mauaji ya kimbari na hata ukiukwaji wa haki za binadamu,
kutokana na hali hiyo kuna haja ya kuboresha mikakati yenu ili kuzuia
kuendelea kutokea kwa mauaji ya kimbari na ukiukwaji wa haki za
binadamu,” alisema.
Aidha, amewaambia wajumbe wa kamati
hiyo kuwa ni jukumu lao kuangalia namna ya kukabiliana changamoto ambazo
zimekuwa zikijitokeza na hivyo kufanya vitendo hivyo kuendelea kuwepo
miongoni mwa nchi za maziwa makuu.
Amewataka wataalamu hao kwenda mbali
zaidi na kubainisha hatua za kisera, kisheria na kiutawala zitakazofaa
kuchukuliwa ili kukabiliana na changamoto ya kuendelea kuwepo kwa
vitendo hivyo, lengo likiwa kuvikomesha ndani ya nchi za ukanda wa
maziwa makuu
0 comments:
Post a Comment