Rais John Magufuli ameyatolea majibu malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini kuwa amekuwa akikandamiza demokrasia tangu alipoingia madarakani.
Akijibu
swali lililoulizwa na mmoja kati ya wahariri wa vyombo vya habari leo
Ikulu jijini Dar es Salaam, aliyetaka ufafanuzi kuhusu malalamiko hayo,
Rais Magufuli alisema kuwa hajawahi kukandamiza demokrasia nchini na
kwamba anachofanya ni kuihuisha.
“Katika
kazi yoyote, critic ni kitu cha kawaida na pongezi ni kitu cha kawaida.
Lakini ukweli ni kwamba katika muda wote ambao nimechaguliwa kuwa Rais
sija-suppress democracy (sijakandamiza demokrasia) na bahati nzuri
ninapromote demokrasia,” alisema Rais Magufuli.
“Na
ndio maana unaona Bunge linaendelea vizuri. Na ndio maana unaona
uchaguzi unafanyika hata hapa Dar es Salaam kuna maeneo wamechagua Ukawa
na kuna maeneo wamechagua CCM. Hiyo ni demokrasia. Mikutano yao ya
ndani ya vyama mmekuwa mkishuhudia, na hivi juzijuzi kumekuwa na mkutano
wa chama fulani, wakagombana wenyewe na wakafukuzana wenyewe,” aliongeza.
Aidha,
akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na mwanahabari mkongwe, Tido
Mhando (Azam TV) kuhusu mtazamo wa baadhi ya watu kuwa huenda anaendesha
mambo kidikteta bila kufuata taratibu zilizowekwa, Rais Magufuli
alisema hiyo ni tafsiri ya mtu ambayo inatokana na uhuru wa kufikiria.
“Kila
mmoja anaweza akatafsiri vyovyote… wewe(Tido) ulipokuwa BBC ukahama
ukaenda TBC, ukahama leo uko Azam, mtu mwingine anaweza akatafsiri kuwa
huenda huo ni udikteta wa namna fulani wa kuhamishwahamishwa. Kwa hiyo
kila mmoja ana uhuru wa kufikiria anavyofikiria,” alisema.
Rais Magufuli leo amefanya mkutano na Wahariri wa vyombo vya habari kwa lengo la kujibu maswali yao
0 comments:
Post a Comment