METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 7, 2016

Mkataba wa EPA pasua kichw

MKATABA wa Uhusiano wa Uchumi na Biashara Kati ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA), umegeuka kaa la moto baada ya mtalaamu wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi, kuainisha vifungu visivyofaa vinavyoweza kuiumiza nchi kama itaukubali.

Kutokana na hali hiyo wabunge wameitaka Serikali isiingie kwa haraka kwenye mkataba huo kwa kuwa hauna maslahi kwa Taifa.

Mkataba huo ambao hadi sasa  Tanzania haijausaini, unatarajiwa kuwasilishwa bungeni Alhamisi wiki hii kwa ajili ya kujadiliwa ingawa Kenya na Rwanda zimekwisha kuusaini.

Akiuchambua mkataba huo    kwenye semina ya wabunge mjini hapa jana, Profesa Kabudi, alisema mkataba huo haifai kwa kuwa una ahadi nyingi zisizotekelezwa.

Kwa mujibu wa mkataba huo, Profesa Kabudi alisema nchi za Ulaya hazitapata hasara yoyote ila nchi za EAC ndiyo itaathirika kwa sababu  hazitaruhusiwa tena kuongeza ushuru wa bidhaa zinazoingia katika nchi husika.

“EPA itasababisha wananchi wa nchi za Afrika Mashariki kukosa ajira kutokana na ukanda huo kugeuka ukanda huru wa bidhaa za Ulaya.

“Kama tutausaini kisha tukataka kuingia kwenye ushirikiano wa uchumi na nchi nyingine zilizo nje ya EPA, mkataba hauturuhusu kwa sababu unalazimisha nchi za EAC  kupeleka kwao bidhaa zenye kuzingatia afya na usalama kwa kukidhi viwango vya nchi zao.

“Kwa mujibu wa mkataba huo, kuna uwezekano bidhaa zetu zikakosa soko kwa kutokidhi vigezo vyao pamoja na kutakiwa kuthibitisha usalama huo kisayansi ambako kwa bidhaa za nchini ni vigumu kupata uthibitisho huo kama asali inayotoka  Tabora.

“Pia, ibara ya 99 ya mkataba huo inakwenda kuua ajira kwa vijana kwa vile  inachagua ni maeneo gani ya kufanyia kazi.

“Uchumi wa nchi yetu sasa tunaelekeza kwenye mkakati wa viwanda, lakini mkataba wa EPA una mtego kwa sababu hausemi ni mazao gani ya biashara yanatakiwa kwao.

“Kwa hiyo, pamoja na Kenya na Rwanda kuusaini, bado katika jumuiya kama kuna mwenzenu mmoja hajasaini, hautasainiwa katika jumuiya husika,” alisema Profesa Kabudi.

Mmoja wa wachambuzi wa mkataba huo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. John Jingu, alisema Tanzania ikisaini mkataba huo, itapoteza mapato kwa sababu inategemea ushuru wa forodha ambao asilimia 10 ya ushuru huo, hutoka kwenye bidhaa zinazoingia kutoka Ulaya.

“EPA itaiathiri Tanzania katika biashara kwa sababu nchi inazofanya nazo biashara si za Umoja wa Ulaya kama vile Saudi Arabia, China, India, Falme za Kiarabu, Afrika Kusini, Uswisi, Marekani, Korea Kusini, Kenya na Andorra.

Awali, Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Adolf Mkenda, alisema Tanzania ikisaini mkataba huo, haitaweza kuongeza kodi na badala yake itabaki na tozo inazotoza.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), alisema  anaunga mkono uchambuzi wa watoa mada kwa sababu  hatua ya kukimbilia kusaini huo ni kuendelea kuumia.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msingwa (Chadema), alisema pamoja na hoja za uzalendo za wachambuzi hao, bado kuna haja ya kuelezwa pia na faida zake badala ya kutajwa hasara peke yake.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliitaka Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, ihakikishe inakutana na timu ya wataalamu wakiwamo wafanyabishara kujadili kwa kina mkataba huo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com