Shirika
la kutetea haki za binadamu Syria limesema leo waasi wa Syria
wamelipoteza eneo lote la kaskazini mwa mji wa Aleppo katika operesheni
inayofanywa na jeshi kuudhibiti kikamilifu mji huo.
Majeshi
ya serikali ya Syria yanadhibiti thuluthi moja ya mji unaodhibitiwa na
waasi wa Aleppo, baada ya mapambano makali mwishoni mwa wiki
yaliyosababisha takriban raia 10,000 kuutoroka mji huo.
Katika
mojawapo ya mafanikio yake makubwa katika azma ya kuudhibiti kikamilifu
mji wa Aleppo, majeshi yaliyakomboa maeneo sita ya mashariki mwa mji huo
mwishoni mwa wiki, likiwemo eneo la Masaken Hanano ambalo ndilo kubwa
mashariki mwa mji huo.
Hapo
jana, siku ya 13 ya operesheni, majeshi pia yaliyadhibiti maeneo ya
Jabal Badra na Baadeen na kuyachukua maeneo mengine matatu. Shirika la
kutetea haki za binadamu Syria limesema majeshi yanadhibiti pia maeneo
mengi ya kaskazini mwa mji huo wa pili kwa ukubwa Syria.
Maelfu ya raia wautoroka mji wa Aleppo
Mkurugenzi
wa shirika hilo la kutetea haki za bindamu Rami Abdel Rahman amesema
waasi wamepoteza asilimia 30 ya maeneo ambayo walikuwa wanayadhibiti
mjini humo na kuongeza kiasi cha raia 10,000 wameutoroka mji huo tangu
siku ya Jumamosi, 6,000 kati yao wakitorokea mji wa kikurdi wa Sheikh
Maksoud na wengine katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali.
Abdel
Rahman amesema hii ndiyo mara ya kwanza kushuhudia idadi kubwa ya raia
wakiondoka Aleppo tangu mwaka 2012. Takriban raia 250,000 waliozingirwa
kwa miezi kadhaa mjini humo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na
mahitaji mengine ya kimsingi.
Yasser al
Youssef wa kundi la waasi la Nureddin al Zinki amesema wapiganaji
wanajaribu kujikusanya katika eneo la Sakhur ili kuulinda mji huo na
wakaazi wake lakini mashambulizi makali ya angani yanaharibu karibu kila
kitu mjini humo.
Kudhibitiwa
kwa eneo la Sakhur, liloko mashariki mwa Aleppo, inamaanisha mji huo
Aleppo utagawanyika mara mbili kaskazini na kusini na kuwa pigo kubwa
kwa upinzani. Kiasi cha raia 225 wakiwemo watoto 27 wameuawa katika
mapambano hayo tangu tarahe 15 mwezi huu.
Majeshi yapania kuudhibiti mji kikamilifu
Umoja wa
Mataifa una mipango ya kufikisha misaada, kuwoandoa walio wagonjwa na
waliojeruhiwa. Waasi wameukubali mpango huo lakini serikali bado
haijaridhia. Hakikisho pia linahitajika kutoka kwa Urusi-mshirika wa
utawala wa Syria.
Wachambuzi
wanasema utawala wa Rais Bashar al Assad unapania kuudhibiti mji huo
wakati huu ambapo sera za kigeni za Marekani zinatarajiwa kubadilika.
Wakati
huo huo, Misri imekanusha taarifa zilizotangazwa katika vyombo vya
habari vya nchi kadhaa za kiarabu kuwa zimetuma majeshi yake nchini
Syria, siku chache baada ya Rais Abdel Fattah al Sisi kutangaza
analiunga mkono jeshi la Syria.
Wizara ya
mambo ya nje ya Misri imesema madai hayo yapo katika fikra za
wanaozikuza taarifa hizo. Mzozo huo wa Syria ambao umedumu kwa miaka
sita sasa umesababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu na mamilioni ya
wengine kuachwa bila ya makazi.DW
0 comments:
Post a Comment