WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya
Dodoma lifanye marekebisho ya kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo
ambayo imepandishwa kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.
Amesema
anatambua maamuzi ya Baraza ni ya kikao halali lakini hakubaliani na
ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati
alipotembelea soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea
huduma za jamii mjini Dodoma.
Amesema
soko hilo linatakiwa lifanyiwe mapitio ili liwekwe kwenye hali nzuri na
Manispaa ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza
wafanyabiashara.
“Kwa
kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na
baraza la Madiwani, sitaki kuvunja sheria. Nawaagiza mkazungumze tena
katika baraza na muangalie namna ya kupunguza gharama hizo,” amesema.
“Hali
hii haiwezekani kuachwa iendelee, huku ni kuwaumiza wananchi.
Mkurugenzi wa Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya
kwenye baraza lenu na mje mnieleze mmekubaliana nini” amesisitiza.
Pia
ameitaka Manispaa hiyo ihakikishe makusanyo yote ya fedha katika soko
hilo yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta
tija na kuwataka Mkuu wa mkoa na wilaya kuwachukulia hatua
wotewatakaobainika kuiba fedha hizo.
Amesema
Manispaa hiyo inatakiwa kupanua masoko kwa kujenga masoko mapya makubwa
katika maeneo ya Nkuhungu, Kisasa, Mlimwa na Barabara ya Iringa ili
huduma hizo zisambazwe.
Mapema
akisoma risala yake, Mwenyekiti wa soko hilo, Bw. Godson Rugazama
alimueleza Waziri Mkuu changamoto zinazolikabili soko hilo kuwa ni
pamoja na ongezeko la kodi isiyozingatia uhalisia wa maisha na shughuli
za wajasiriamali sokoni hapo. “Kodi imeongezeka kutoka sh. 20,000 hadi
150,000 kwa mwezi,” alisema.
Mwenyekiti
huyo alitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa mifereji ya maji
machafu, kuvuja kwa paa la soko, bidhaa kuuzwa katika maeneo yasiyokuwa
rasmi na kusababisha wateja kutoingia sokoni.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu ametembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma na
kukagua maeneo mbalimbali zikiwemo wodi za wagonjwa, jengo la wazazi na
jengo jipya la wagonjwa wa Bima ya Afya (NHIF).
Akiwa
hospitalini hapo, pia alizungumza na watumishi wa sekta ya afya na
kuwataka wawahimize wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF)
ambao unawawezesha mtu kulipia bima ya matibabu kwa ajili ya mhusika,
mwenza wake na watoto/watemezi wanne na serikali inajazia kiasi kile
kile alichochangia.
Akizungumzia
miundombinu ya afya mkoani humo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa Dodoma
hauna shida ya matibabu au utoaji wa huduma ya afya kutokana na
miundombinu iliyopo hivi sasa.
Aliwataka
wafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu na kuongeza tija katika utendaji
kazi wao huku wakitanguliza utunzaji wa mali ya umma.
“Ninawasihi
mjenge tabia ya huruma kwa wagonjwa huku mkitambua unyeti wa kazi
mliyonayo. Ninaamini mtatunza vifaa mlivyonavyo na siyo kuvichukua na
kuvipeleka kwenye zahanati zenu au maduka yenu binafsi ya dawa,”
alionya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Post a Comment