BAADHI ya wadau wakuu wa Tasnia ya Habari wameendelea kugomea kutoa
maoni yao mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya
Jamii, kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari wa mwaka 2016, baada
ya ‘kukacha’ kuhudhuria kikao maalumu cha kamati hiyo cha kupokea maoni
yao, huku Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kikiwasilisha maoni
yake.
Kutokana na TLS kuwa wadau pekee waliowasilisha maoni yao, Kamati
hiyo ya Bunge jana iliyapitia maoni hayo na kuyajadili kifungu kwa
kifungu kwa ajili ya kuboresha muswada huo.
Kamati hiyo ilitakiwa kusikiliza maoni ya wadau hao katika mkutano
uliofanyika mjini Dodoma jana, ambapo waliwasilisha barua za kushindwa
kuhudhuria kikao hicho na kushauri muswada huo, usogezwe mbele badala ya
kuwasilishwa katika Bunge lijalo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba, alisema kamati hiyo
imepokea baadhi ya barua za wadau hao ambao ni Baraza la Habari Tanzania
(MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), MISA Tan na
Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) wakiitarifu
kamati hiyo kuwa hawatahudhuria wala kutoa maoni yao.
“Kwa mujibu wa barua hizi, wadau hawa wamekiri kupokea mwaliko wetu
wa kamati lakini wamesisitiza kuwa hawatohudhuria kwa kuwa wanaamini
muswada huo bado unahitaji kusogezwa mbele zaidi,” alisema Serukamba.
Alisema, mapema wiki iliyopita kamati hiyo iliwapatia muda wa
takribani siku tisa wadau hao ili waweze kujiandaa na kutoa maoni yenye
tija, baada ya kuwasilisha kilio chao kuwa muda waliopewa kupitia
muswada huo hautoshi.
“Pamoja na ukweli kuwa muswada unaposomwa kwa mara ya kwanza bungeni
unakuwa uko wazi kwa wadau na wananchi, tuliwapatia muda wajipange zaidi
kama walivyoomba,”alisisitiza.
Alisema kimsingi kanuni za Bunge, zinabainisha kuwa muswada
unaposomwa kwa mara ya kwanza bungeni, kila mwananchi au mdau
anayehitaji kuusoma anaupata kirahisi.
“Kwa muda uliosomwa muswada huu Septemba, mwaka huu, wadau hawa
walikuwa na muda wa kutosha kuupitia na kutoa maoni yao,” alisema.
Alisema mara baada ya kusomwa kwa muswada huo, si kazi ya Bunge
kuwaita wadau na kuwashawishi wausome muswada huo, bali ni utashi wao
ndio unaosukuma kuutafuta, kuusoma na kutoa maoni yao kwa Kamati ya
Bunge kwa mujibu wa taratibu.
“Kazi yetu sisi Bunge kupitia kamati ni kuwaita wadau watoe maoni
yao, ambayo tunayapitia na kujadili na kuyawasilisha kwa Bunge kwa
kuishirikisha serikali na kuboresha zaidi muswada,”alifafanua.
Serukamba alisema hiyo si mara ya kwanza kwa wadau wa habari,
kuendelea kukwamisha muswada huo usisomwe bungeni, kwani kwa takribani
miaka 23 iliyopita, umekuwa ukikwama kuwasilishwa kutokana na migomo ya
wadau hao wakiomba muda zaidi.
“Kila mara unapofikia hatua nzuri ya kuwasilishwa bungeni, wadau
wanakataa kwa madai kuwa hawako tayari na kuomba usogezwe mbele, sasa
wamefanya jambo hili kama ni mchezo. Sasa sisi tunasema kama kukataa
kwao kutoa maoni ni njia ya kuonesha wanaukubali lakini wanaficha sura
zao au wanaukataa, sisi tutasonga mbele,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo alisema kamati hiyo, kwa sasa inapitia maoni ya wadau
wengine, yaliyowasilishwa kwa njia ya barua na barua pepe, ambayo
yatajadiliwa na kujumuishwa kwenye mapendekezo ya kamati hiyo kwa ajili
ya kufanyiwa kazi zaidi.
Hicho ni kikao cha pili cha kamati hiyo cha kukusanya maoni ya wadau,
ambapo kikao cha kwanza kilifanyika mapema wiki iliyopita, lakini wadau
hao wakiongozwa na Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari (MOAT),
walishindwa kuwasilisha maoni na kuomba wapatiwe muda wa miezi minne ili
waupitie vyema muswada huo.
Wadau waliohudhuria kikao hicho na kuomba kuongezewa muda ni Jukwaa
la Wahariri (TEF), klabu mbalimbali za waandishi wa habari, MCT,
MISA-Tan, LHRC na TLS.
Sunday, October 30, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. ...
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. 4, 000,000,000/= kutoka kwa Meneja Mkazi (Country Manager) wa Kampuni ya Madini ya...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua kikao kazi cha vyama vya ushirika kuhusu ununuzi wa mbolea k...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment