SIKU chache baada ya gazeti hili kuchapisha ripoti maalumu kuhusu
mauaji ya tembo katika Pori la Akiba la Selous na matokeo ya Operesheni
Tokomeza Ujangili, mmoja wa waliokuwa washukiwa wa matukio hayo
amejitokeza na kueleza maswahibu yaliyomkumba.
Dereva wa zamani wa treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA), Mahyoro Ismail, ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam,
amesema vita ya mapambano ya kuokoa tembo ndani ya Pori la Selous,
imemsabishia ulemavu wa baadhi ya viungo.
Mbali ya madhara hayo, ameeleza kushindwa kulipa Sh milioni 32 za
mkopo wa trekta aliokopa kutoka katika Mfuko wa Pembejeo mwaka 2013 na
pia kushindwa kurudishiwa bunduki yake na risasi 15 zilizochukuliwa
nyumbani kwake baada ya kukamatwa na kuhusishwa na mauaji ya tembo
katika Pori la Selous.
Mahyoro aliyeendesha treni ya Tazara kuanzia mwaka 1977 na kustaafu
mwaka 2003, alisema aliamua kukopa trekta kutoka Mfuko wa Pembejeo mwaka
2009 lakini aliweza kupewa trekta hilo na jembe lake mwaka 2013, akiwa
na lengo la kulitumia katika kilimo katika eneo la Kisaki, lililo
pembezoni mwa pori hilo.
Alisema trekta alilokopa lilikuwa na thamani ya Sh milioni 26.8 na
alitakiwa kulipa katika kipindi cha miaka minne na kutakiwa kulipa Sh
milioni 32 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, jambo ambalo sasa linamuweka
katika mazingira magumu kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipa deni
hilo.
Akikumbushia kilichompata Mahyoro alisema kamwe hawezi kuusahau usiku
wa Oktoba 28, 2013 saa 7.30 usiku, ambapo alivamiwa na askari akiwa
katika mashamba yake katika eneo hilo la Kisaki na kuelezwa kuwa alikuwa
anahusika na mauaji ya tembo katika Pori la Selous.
“Nakumbuka ilikuwa saa 7.30 usiku. Nikiwa chumbani ghafla niliona
tochi kubwa inanimulika kutokea dirishani. Nilishtuka sana na ghafla
nilisikia watu wakijitambulisha kuwa ni askari na kuniamuru nifungue
mlango, kwa vile nahusika na mauaji ya tembo,” alisema.
Alisema pamoja na madai hayo kwake, askari hao waliomtuhumu pia kuwa
anamiliki silaha mbalimbali zinazotumika kuua tembo ndani ya pori hilo,
walimfanyia upekuzi na kushindwa kupata silaha yoyote katika nyumba yake
ya shambani Kisaki hadi walipomsafirisha siku kadhaa baadaye kwenda
nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kuikuta bunduki aliyokuwa
anaimiliki kihalali aina ya Rifle 458 Manlicher yenye namba 18243 na
risasi 15.
Pamoja na kueleza madhara mbalimbali yaliyompata baada ya kukamatwa
kwake na kushikiliwa kwa siku kadhaa katika Kambi ya Matambwe liliko
lango kuu la kuingilia ndani ya Pori la Selous, Mahyoro alisema tukio
hilo limemfanya kubaki na ulemavu wa baadhi ya viungo na hasara kubwa.
Sakata la bunduki
Akizungumzia mwito uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Mwigulu Nchemba alipozungumza na gazeti hili hivi karibuni kwamba
walionyang’anywa bunduki katika Operesheni Tokomeza wafike katika vituo
vya Polisi wakiwa na leseni zao ili warejeshewe, Mahyoro alisema agizo
hilo la Waziri linakabiliwa na vikwazo kadhaa.
“Tunashukuru Waziri (Mwigulu) kupitia gazeti lenu (HabariLeo)
ameagiza tufike na leseni zetu kuchukua bunduki zetu, lakini sisi
wengine tulinyang’anywa bunduki na leseni yake na kwa muda mrefu sasa
mimi binafsi nimekuwa nafuatilia bunduki yangu lakini nimekuwa
nazungushwa bila kupata msaada wowote,” alisema.
Mbali ya kuelezea hatua alizozipitia, Mahyoro aliweza kuonesha barua
mbalimbali na majibu juu ya kumtaka kuendelea kuvuta subira wakati hatua
za kuisaka bunduki yake zikiendelea zikiwemo barua tatu kutoka Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Barua hizo ni pamoja na ya Agosti 10,2015 iliyosainiwa na Veronica
Chacha ambaye ni Wakili wa Serikali Mfawidhi, ya Septemba 8, 2015
iliyosainiwa na Calistus Kapinga na ile ya Februari 24, mwaka huu
iliyosainiwa pia na Kapinga, ambazo zote zinamtaka kuendelea kuvuta
subira wakati suala la upatikanaji wa bunduki hiyo likifanyiwa kazi.
Barua nyingine ni ile ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya Agosti 4,
mwaka huu, iliyosainiwa na Keraryo H.W inayomtaka pia kuendelea
kusubiri; hatua ambayo Mahyoro alisema inatia shaka agizo la Waziri
Mwigulu kutekelezeka, huku akimuomba Waziri huyo kumsaidia aweze kupata
bunduki hiyo.
Sakata la Mkopo
Alisema tukio la kukamatwa kwake pia lilisababisha madhara makubwa
kwani aliporejea alibaini trekta alilokuwa amekopa kutoka Mfuko wa
Pembejeo kuibiwa vifaa mbalimbali nyumbani kwake Kisaki na kutokana na
ukosefu wa fedha za kununua vipuri vilivyoibwa hadi sasa ameshindwa
kuendelea na shughuli za kilimo na hivyo kukosa fedha za kurejesha
mkopo.
Sunday, October 30, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. ...
-
Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samuel Jeremia Opulukwa akinawa mikono kabla ya kuingia katika Zahanati ya Saza itakayotumika kutibu endapo ata...
-
MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania (DCI), Robert Boaz Mikomangwa amesema Jeshi la Polisi nchini Tanzania na vyombo vingi...
-
Naibu waziri Kilimo Mhe. Omari T. Mgumba (Mb) akiwa ofisi ya mkuu wa mkoa wa arusha alipokutana na wataalamu wa kilimo ,ushirika na ...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment