METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 22, 2016

Stars Supporters inavyobebwa na Platinum

KWENYE mpira wa miguu inasemwa kwamba shabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani.

Kwa maana anavyoshangilia zile kelele zinaongeza hamasa kwa wachezaji. Tanzania huwa kuna tatizo la ushangiliaji, mashabiki wa soka wamezoea kushangilia pale tu linapofungwa bao au mchezaji wa timu husika anaposhambulia lango la wapinzani. Tatizo hili lipo pote si kwenye timu za taifa wala kwenye klabu. Tena kwenye timu ya taifa ndio kabisa mashabiki wanaweza kuanza kusomea ama kushabikia timu pinzani kisa tu timu yao inacheza vibaya siku hiyo.

Ilipokuja timu ya TP Mazembe kucheza na Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2011 hamasa ya ushangiliaji ilianzia pale. Mashabiki wa Tanzania walifurahi jinsi vikundi vya ushangiliaji vilivyokuwa vikishangilia kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo mpaka ya mwisho.

Hawakuwa wakiwafikia wale wa Liverpool lakini angalau walikuwa wakishangilia na kuwafanya wachezaji wao kujiona wako pamoja uwanjani.

Ndipo baadhi ya mashabiki wa soka nchini walipoamua kuanzisha kikundi cha hamasa kwa timu za taifa ambapo kilianza mwishoni mwa mwaka jana. Kundi hilo linalojulikana kama Taifa Stars Supporters limekuwa likihamasishana kusafiri na timu za taifa nje ya nchi zikiwa na vigoma vyao kwa ajili ya kuzishangilia na hakika limekuwa kundi muhimu kwa timu za taifa kuanzia za vijana mpaka za wakubwa kwa upande wa wanawake na wanaume.

Hata hivyo, kikundi hicho kimekuwa hakina mtu wa kukipa msaada zaidi ya kuchangishana wenyewe kufanikisha safari za kwenda uwanjani, kupokea timu uwanja wa ndege au kusafiri kwa nchi za karibu kama Zambia, Kenya, Uganda. Ndipo kampuni ua Platinum Credit inayohusika na mikopo ilipoamua kujitosa kusaidia kikundi hicho japo kwa kutoa fulana kwa ajili ya wanachama wake.

“Tunawashukuru sana Platinum Credit kwa moyo wao wa kizalendo ambao wamekuwa wakitusaidia ili tuweze kutimiza majukumu yetu ya kuzishangilia timu zetu za Taifa, kama wote tunavyojua ushangiliaji ni moja ya sehemu ya uchezaji ambao unachochea matokeo mazuri uwanjani… “Kikundi chetu ndio kiko kwenye kujijenga nia nikurudisha uzalendo uliokuwa umepoa kwenye michezo, hivyo wadau mbalimbali wajitokeze kuhakikisha kwamba tunakuwa na moyo na kuzipenda timu zetu za Taifa ambazo kiukweli kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha zinafanya vizuri kwa maslahi ya- Taifa,” ndivyo anavyoanza kusema Mwenyekiti wa kundi hilo Godson Karigo katika mahojiano maalumu na gazeti hili.

Anasema ilitokea tu walikutana mashabiki wachache wa soka wakaamua kuja na kitu hicho ili kurudisha morali ya mashabiki wa soka kwa kushangilia timu zao na kweli jambo hilo likafanikiwa.

“Kwanza tulianza kwenye kuunda kundi la Whatsap, humo ndipo tulipokuwa tukijadili namna ya kufanya, kundi hilo kila mtu anayejisikia kuwa mwanakikundi anatoa namba yake anaungwa, tulijadiliana na mwisho tukafanya mkutano wa kwanza ambapo baadae tukatengeneza katiba na kusajili umoja wetu, kwa hiyo tupo kihalali na tumesajiliwa,” anasema.

Sasa kikundi hicho maarufu chini ya Mwenyekiti Karigo kimekuwa kikionesha uzalendo wa hali ya juu katika ushangiliaji wa timu za Taifa bila kujali aina ya matokeo uwanjani. Ni wazi kwamba kuwepo kwa kikundi hicho kimeongeza hamasa kubwa na kuibua uzalendo upya kwa wananchi na sasa imeanza kuwa kawaida kuona watanzania wakiendelea kushangilia timu zao mwanzo wa mchezo hadi mwisho.

Mara zote unapokuwa uwanjani kikosi hicho kimekuwa kikitoa hamasa mwanzo wa mchezo hadi mwisho, kitu ambacho hakikuwepo kabisa katika soka la hapa nyumbani. Akizungumza na namna wanavyoendesha kikosi hicho, Karigo anasema mara nyingi wamekuwa wakijitolea kuhakikisha vijana wanawezeshwa kufika katika eneo la kutoa hamasa iwe uwanjani kwa ajili ya mechi au uwanja wa ndege kupokea timu inaporejea kutoka nje ya nchi kushiriki michuano mbalimbali.

“Mpaka sasa bado tunaendesha kikundi kwa kuchangishana pesa kutoka mifukoni mwetu nia yetu ni kuhakikisha timu zetu kujituma na kujua kwamba zina deni kwa watanzania ambao tuna kiu ya kuhakikisha siku moja tunafanikiwa sana kisoka,” anasema. “Ndio maana hata timu zinapokuwa zinacheza mechi zake nchi za jirani tunaanza kuchangishana na kuisindikiza timu, hii yote lengo lake ni kuhamasisha soka letu”.

“Tunaomba wadau wengine wengi wajitokeze kuunga mkono juhudi za hiki kikundi ambacho kwa sasa kina vijana wanaozidi 400 wako tayari kutumika kuhamasisha... “Ukifuatilia mafanikio ya vikundi vya ushangiliaji kwenye timu za Taifa za wenzetu utaona ambavyo vimechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa matokeo mazuri, mpira unachezwa uwanjani na wachezaji 11, lakini jukwaani huwa kunahesabika ni mchezaji wa 12 kwani inaaminika kabisa ushangiliaji ni chachu ya ushindi”.

Katika mapokezi ya timu ya soka ya Taifa ya wanawake iliyochukua ubingwa wa Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika Jinja, Uganda, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo Nape Nnauye anasisitiza wadau kujitokeza katika kuhamasisha timu za Taifa ikiwemo ushangiliaji ambao unaongeza hamasa katika kuleta mafanikio kwenye soka.

Nape alionyesha kuvutiwa zaidi na juhudi zinazofanywa na kikundi cha stars Suportes kwa kujituma kuzishangilia timu za Taifa ambazo kwa hakika mafanikio yake ni faida kwa nchi nzima. Kwa kuonesha kwamba anaunga mkono kikundi hicho alimwahidi shabiki maarufu wa ushangiliaji katika michuano ya Ndondo maarufu kama Chifu kwamba aandae hati ya kusafiria ili awe anasafiri na timu za taifa ikienda nchi jirani.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com