Mkazi
wa Machimbo Yombo jijini Dar es Salaam, Salum Njwele (34) maarufu kama
Scorpion, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu
mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumtoboa macho yote mawili
Said Mrisho.
Scorpion
alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore
na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Munde Kalombola.
Akisoma
mashitaka hayo, Kalombola alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo
Septemba 6, mwaka huu eneo la Buguruni Sheli wilaya ya Ilala.
Munde
alidai, Njwele aliiba mkufu rangi ya fedha wenye uzito wa gramu 34
ikiwa na thamani ya Sh 60,000, bangili na fedha taslimu Sh 331,000 vyote
kwa pamoja vikiwa na thamani ya Sh 476,000 mali ya Mrisho.
Kalombola
alidai kuwa mshitakiwa kabla na baada ya wizi huo, alimchoma kisu
machoni, tumboni na mabegani mlalamikaji ili ajipatie mali hizo.
Hata hivyo, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na upande wa mashitaka uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja.
Hakimu
Sachore aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 19, mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena. Mshitakiwa alirudishwa rumande kutokana na mashitaka
yanayomkabili kutokuwa na dhamana.
0 comments:
Post a Comment