Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
14 Oktoba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa
Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe.Qian Keming ambapo viongozi hao
wamekubaliana kuharakisha miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano wa nchi
hizo mbili ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kati.
Katika
mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Rais Magufuli
amemueleza Mhe. Qian Keming kuwa Serikali yake ya awamu ya tano inataka
kuona mambo yakifanyika na kutoa matokeo bila kupoteza muda na kwamba
angependa wadau wa maendeleo hasa nchi ya China ambayo ni ndugu na
rafiki mkubwa wa Tanzania iende katika kasi hiyo hiyo.
Rais
Magufuli ameuzungumzia mradi wa ujenzi wa reli ya kati ya kutoka Dar es
Salaam, Mwanza, Kigoma na kuunganisha nchi za Rwanda na Burundi ambao
Tanzania imetenga Shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi
katika bajeti hii, kwa kutaka China ambayo imekubali kushiriki katika
ujenzi iendane na kasi ya Serikali yake.
“Mhe.
Qian Keming sisi tumeamua kuanza ujenzi na tayari Wakandarasi 32
wamejitokeza kuomba kujenga reli ya kati kuanzia Dar es Salaam hadi
Morogoro umbali wa kilometa 200 za mwanzo na tutatumia fedha zetu
wenyewe.
“Kazi
hii tunataka ianze mwaka huu wa fedha, kwa sababu upembuzi yakinifu na
usanifu umeshafanyika, kwa hiyo na nyie ongezeni kasi ili mradi huu wote
ukamilike, nataka uwe umekamilika kabla sijaondoka madarakani” amesema Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli ameongeza kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa Tanzania na
nchi nyingine nane zinazotegemea bandari ya Dar es Salaam na kwamba
kukamilika kwake kutatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa
Tanzania ambayo imedhamiria kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka
2025.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Biashara wa China Mheshimiwa Qian Keming
amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kukuza uchumi wa
Tanzania, kupiga vita rushwa na kwa namna ya kipekee kwa dhamira yake
ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na China na ameahidi kuwa
Serikali ya China itaongeza msukumo katika uharakishaji wa utekelezaji
wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kati.
“Mheshimiwa
Rais Magufuli nimeielewa dhamira yako na kiu uliyonayo, naona kabisa
kwamba dhamira ya kisiasa ipo ya kutosha, tunachotakiwa kukifanya ni
kuwasukuma wataalamu wetu waongeze kasi, na mimi nakuahidi kuwa tulikuwa
tunakwenda kwa kasi ya kilometa 100 kwa saa, sasa tutaongeza na kwenda
kilometa 200 kwa saa” amesema Mhe. Qian Keming.
Mazungumzo
hayo yamehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing,
Makamu wa Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Sun Ping, Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles John Mwijage na Waziri wa
Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Oktoba, 2016
0 comments:
Post a Comment