Inatarajiwa kuwa jumla ya wahamiaji 2,500 watakuwa wamehamishwa kufikia mwisho wa leo.
Ufaransa
imeanza kuwaondoa wahamiaji waliopo katika kambi ya Calais kwa lengo la
kuifunga kambi hiyo ya porini. Shughuli hiyo inafanywa huku polisi
waliojihami wakishika doria. Usiku wa kuamkia leo kulikuwa na
makabiliano kati ya polisi na baadhi ya makundi madogo ya wahamiaji
walipoteketeza vyoo wakipinga mpango wa kambi hiyo kufungwa.
Mabasi ya
kwanza yaliyowabeba wahamiaji kuwaondoa katika kambi ya Calais yalianza
safari mapema leo, muda mfupi tu baada ya maafisa wa uhamiaji kuanzisha
operesheni hiyo. Mamia ya wahamiaji walionekana wakipiga foleni
wakibeba mabegi yao ili kufanyiwa ukaguzi tayari kuhamishwa hadi katika
vituo vingine 450 nchini Ufaransa.
Inatarajiwa
kuwa kufikia mwisho wa leo, jumla ya wahamiaji 2,500 watakuwa
wamehamishwa kutumia mabasi 60 yanayotarajiwa kuwabeba leo. Fabienne
Bucco ni meya katika eneo hilo na anasema "Inaendelea salama, tulijua
asubuhi hii kutakuwa na watu wengi, na ndiyo inayofanyika, kulikuwa na
mamia ya wahamiaji wakisubiri banda kufunguliwa. Tulifungua saa
tuliyopanga, kila kitu kikafanyika kiutulivu, hakukuwa na msukumano,
watoto walifika taratibu. Tulikuwa na wasiwasi haswa kwa watoto,
tukawapa kipaumbele, lakini kila kitu kimeenda shwari".
Serikali
ya Ufaransa inasema inafunga kambi hiyo inayowahifadhi watu 6,500,
waliotoroka vita na umaskini katika nchi zao, kwa misingi ya kibinadamu.
Ufaransa inatarajia kumaliza kuwahamisha wahamiaji hao wote kufikia
mwisho wa wiki hii, kisha wiki kesho, ianze kuibomoa na kuifunga kabisa
kambi hiyo.
Japo
utulivu umeshuhudiwa operesheni ilipong'oa nanga, maafisa wanaotoa
misaada wanahofia huenda mamia ya wahamiaji wengine watakataa kuondoka,
hivyo kuonya kuwa huenda kukatokea vurugu baadaye shughuli ya kuibomoa
kambi itakapoanza.
Lakini
hata operesheni ya kuwahamisha inapoendelea, hatima ya watoto-wahamiaji
1,300 ambao wako kivyao kwa kuwa hawakuandamana na wazazi wao
haijulikani bayana. Siku ya Ijumaa wiki jana, waziri wa usalama wa ndani
ya Ufaransa alisema mazungumzo yanaendelea kuhusu nani anapaswa
kuwachukua watoto hao wasiokuwa na uhusiano na wazazi nchini Uingereza.
Ni watoto
sabini tu wamehamishiwa Uingereza kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu na
mapema mwezi wa Oktoba kabla ya kuanza kutekelezwa kikamilifu kwa mpango
wa kuibomoa kambi hiyo. Uingereza imekuwa ikishutumiwa kwa kuburuza
miguu katika mchakato huo lakini Ufaransa nayo pia inakoselewa kwa
kuukwamisha mchakato huo kwa kushindwa kuwasilisha kesi za kutosha za
kuzingatiwa.
Mashirika
ya hisani ya Uingereza na wabunge wamemwandikia waziri wa mambo ya
ndani wa Ufaransa Benard Cazeneuve kufafanuwa kile wanachosema "wasi
wasi mkubwa kuhusiana na usalama na hali ya watoto wasioandamana na
wazazi wao na watu wazima wanyonge au wasiojiweza.
Mashirika
hayo yakiwemo shirika lisilo la kiserikali la Kuwaokowa Watoto la Save
the Children ,Baraza la Wakimbizi na Kamati ya Kimataifa ya Uokozi ya
Msalaba Mwekundu nchini Uingereza yameandika kwamba "rasilmali
zinazotumika hivi sasa hazitoshi kuhakikisha ulinzi wa uhakika kwa watu
walioko hatarini kabisa hususan watoto wasioandamana na familia zao".
Barua yao
imeonya kwamba kuvunjwa kwa kambi bila ya mandalizi makini kutawaweka
katika mazingira ya hatari zaidi wale ambao tayari wako hatarini.
Operesheni
ya kuwahamisha wahamiaji hao inafanywa chini ya ulinzi wa maafisa wa
polisi waliojihami. Usiku wa jana, baadhi ya wahamiaji waliteketeza moto
vyoo katika kambi hiyo na kuwarushia polisi mawe kama njia ya kupinga
mpango wa kuondolewa kwao.
Wengi wa
wahamiaji na wakimbizi hao waliotoka nchi za Afghanistan, Syria na
Eritrea, wamekuwa wakitaka kufika Uingereza, lakini bila mafanikio
kufuatia sheria za Umoja wa Ulaya zinazotaka kuwa kwanza watafute
hifadhi katika nchi ya Ulaya waliyotangulia kufika.DW
0 comments:
Post a Comment