METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 5, 2016

Neno La Leo: " Enyi Walimu Watakatifu.."



Ndugu zangu,
Leo ni Siku ya Mwalimu Duniani.
Inabaki, kuwa dhumuni kubwa la maisha ya mwanadamu ni kufanya juhudi za kutafuta namna ya kuyaelewa mazingira yake na hivyo kupiga hatua za maendeleo.

Na juhudi hizo za mwanadamu ndicho chenye kujulikana kama ' Elimu'. Naam, mwanadamu anapaswa aitafute elimu, hivyo basi, maarifa.
Na shule yaweza kutafsiriwa kuwa ni ' Maabara' ambamo hutengenezwa ' chanjo' ya maradhi ya kimaisha kwa mwanadamu. Wale wenye maarifa na busara za kuandaa ' chanjo' hiyo ndio wanaoitwa walimu.

Maana, shule ni mahali pa kujifunzia, ambapo yote yenye kuhusiana na maisha ya sasa na hata yajayo hufundishwa. Ni mahali ambapo hupatikana tafsiri za vitu na matukio katika jamii. Ni mahali ambapo, mbali ya mambo mengine, mwanafunzi anapaswa kusaidiwa kuweza kupata maarifa ya kujitambua na kuyatambua mazingira anamoishi.

Twaweza kabisa kusema, kuwa shule ni mahali pa ' ibada'. Na ' viongozi watakatifu' wenye kupaswa kuongoza ' ibada' hizo ni WALIMU.
Hivyo, enyi walimu ' watakatifu' , mnapaswa kuianza sasa kazi ya kuitambua nafasi yenu katika jamii. Vile vile, kulitambua jukumu lenu, vinginevyo, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa kwenye elimu, yumkini yaweza kuwa sawa na mkulima anayesubiria ' mavuno' makubwa sasa ilihali shamba alilolima ni dogo. Amepanda mbegu dhaifu na ameshindwa hata kupalilia shamba lake.
Ni Neno La Leo.
Maggid,
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com