METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 16, 2016

mwenkiti-wa-kijiji

Na Mwamvua Mwinyi,Vigwaza

DIWANI wa kata ya Vigwaza ,wilayani Bagamoyo mkoani Pwani,Muhsin Baruhan ametoa msaada wa madawa ya magonjwa mbalimbali katika zahanati mbili ya Vigwaza na Ruvu Darajani,yenye thamani ya mil.4.5.

Diwani huyo ametoa madawa hayo kwa lengo la kupunguza makali ya uhaba wa madawa unaokabili zahanati hizo na shirikiana na serikali kutatua changamoto zinazokabili sekta ya afya.

Aidha Baruhan ametoa msaada mwingine wa matofali 1,000 pamoja na mifuko ya saruji 30 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba ya mganga mfawidhi wa zahanati ya Ruvu Darajani .

Akikabidhi misaada hiyo ,katika zahanati hizo,alisema ataendelea kutatua matatizo yanayowakabili wakazi wa kata ya Vigwaza kwenye afya,maji,elimu na kusaidia makundi maalum ikiwemo vijana,walemavu ,wanawake na wazee.

Alisema fedha zilizotumika kununulia madawa ,mifuko ya saruji na matofali ni nguvu yake mwenyewe na ni moja ya ahadi zake alizoahidi kuzitatua.
Baruhan alieleza kuwa kwasasa watumishi wa afya katika zahanati hiyo wanaishi katika nyumba za kupanga na kupata kero hasa nyakati za usiku kukitokea mgonjwa wa dharura .
 
Aliomba wadau wa maendeleo,wa afya wajitokeze kushirikiana kujenga nyumba hiyo ili kuondoa kero ya kuishi mbali ya kituo kwenye nyumba za kupanga.

“Tulipiga kelele sana kwenye baraza la madiwani kuhusu zahanati hii kuingizwa katika mgao wa MSD ,tunashukuru mungu katusikia na sasa tumeingizwa katika mgao wa madawa wa kusaidia na serikali”alisema Baruhan.

Baruhan alishukuru serikali na kuiomba ipeleke dawa kwenye zahanati kwa wakati ili wananchi wasihangaike .

Alimuomba mganga mfawidhi katika zahanati ya Ruvu Darajani,afisa mtabibu zahanati ya Vigwaza,kuyatunza madawa hayo kwani yanagharimu fedha nyingi.

“Kipindi hiki ni kigumu kiuchumi, dawa hizi zitumike vizuri,ningeweza kuanzisha duka la vipodozi ama la madawa lakini nimeona umuhimu wa kushirikiana na jamii ambayo ilinijali kwa kunichagua ili iweze kunufaika na kuondokana na kero ya kununua madawa kwenye maduka ya nje ya vituo”alisema.

Nae mganga mfawidhi wa zahanati ya Ruvu Darajani,Gilbert Mkotigwa,alisema zahanati hiyo ilikuwa haijaingizwa katika mgao wa dawa kutoka bohari ya madawa (MSD)kwa miaka mitatu iliyopita tangu feb 2014 hadi sept 5 mwaka huu.

Alisema katika kipindi hicho walikuwa wakisaidiwa na zahanati za jirani ikiwemo Visezi,Kidogozero,Milo,Vigwaza pamoja na wilaya ambayo ilikuwa ikitupa mgao kutokana na fedha za OC.

Dk,Mkotigwa alisema kutokana na uhaba huo ndio uliomsukuma diwani kuomba orodha ya madawa wanayoyahitaji ambapo amewasaidia.
 
Alisema licha ya kupokea msaada huo lakini bado zahanati inakabiliwa na matatizo mengine ikiwa ni sanjali na ukosefu wa nyumba ya mganga na watumishi,wodi ya uzazi kwani kwa sasa wanaojifungua wanajifungulia katika chumba kidogo ,mashine za kupimia wingi wa damu,sukari na haja kubwa.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa chumba cha maabara,wazee wa kijiji kutoingizwa katika mpango wa mfuko wa kusaidia wazee na kaya maskini(TASAF).

Dk.Mkotigwa alisema kukosekana kwa mashine ya kupimia wingi wa damu kunasababisha wajawazito kwenda kupima wingi wa damu kituo cha afya Mlandizi ambayo imekuwa kero kwa wajawazito kufuata huduma hiyo mbali huku ikiwa ni kipimo muhimu kwao tangu kushika mimba hadi kujifungua.

Alimuomba diwani huyo kushirikiana na wahisani wengine kuangalia namna ya kusaidia upatikanaji wa vipimo hivyo na kutafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kutoa huduma bora .

Alisema zahanati hiyo inahudumia wagonjwa wa ndani na nje 400-500 kwa mwezi na wajawazito 10 hadi 15 katika kipindi hicho.
 
Afisa tabibu wa zahanati ya Vigwaza ,Alexander Ngalawa ,alisema zahanati hiyo ina hudumia vijiji vitano na ipo karibu na barabara kuu ya Morogoro-Dar-es salaam hivyo watu wengi kukimbilia kupata huduma ya afya.

Alisema bado wana upungufu wa madawa ,unaotokana na kupelekewa upungufu wa madawa wanayooda kupitia wilaya kwenda bohari na kusababisha upungufu katika mahitaji yao.

Dk.Ngalawa alieleza kwenye zahanati hiyo wapo watumishi watatu ambao hawatoshi ,mmoja akipata likizo wanabaki wawili hivyo kuhemewa na wagonjwa .

Alimshukuru diwani wa kata ya Vigwaza kwa kutoa msaada wa madawa na kuahidi kuzitumia vizuri kwa utaratibu unaotakiwa .

Mkazi wa kijiji cha Vigwaza Zulfa Hassan alisema madawa hayo yatasaidia hasa watoto ,wazee na akina mama .

Alisema awali walikuwa wakipata shida ya kwenda nje ya kata kununua madawa lakini kwasasa watapata unafuu kupata dawa katika zahanati husika.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com