METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 5, 2016

Muswada wa kuweka masharti ya ualimu waja


Serikali  inakamilisha Muswada wa Sheria utakaoweka wazi sifa za walimu wakiwamo wa vyuo vikuu, msingi na sekondari nchini.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi , Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako katika kongamano la kujadili hali halisi ya elimu nchini lililoandaliwa na walimu wastaafu.
Profesa Ndalichako alisema   serikali pia inaandaa  mpango wa kuanzisha chombo maalum cha kitaaluma kitakachosimamia walimu kwa mujibu wa sheria.

Alisema muswada huo utakapokuwa tayari utawasilishwa bungeni.

Alisema  pamoja na mambo mengine, utataja sifa za mwalimu mkuu na mkuu wa chuo  kuondoa dhana kwamba ualimu ni kazi ya walimu mazoea.

“Ni lazima kuwe na sheria inayoweka wazi sifa ya mwalimu mkuu wa chuo kikuu na sifa za kuweza kujiunga na chuo cha ualimu.

“Siyo kuweka tu sheria zisizojieleza hali ambayo imesababisha taifa kuwa na wasomi wasiokuwa na sifa.

“Ili tuweze kufikia katika mpango wa kutoa elimu bora ni lazima tuchukue hatua zinazostahiki kwa manufaa ya taifa ingawa unapochukua hatua Watanzania wengi wanalalamikia suala hili ila ukweli utabaki kuwa ukweli.

“Nchi haiwezi kuendeshwa na walimu wasiokuwa na sifa kwa sababu kitakachozalishwa pia kitakuwa ni mtihani na aibu kwa nchi.

“Kama kuna mwalimu yeyote ambaye anajijua hana sifa na amekalia kiti hicho kwa zaidi ya miaka 10 atambue kuwa hicho kiti atakiacha.

“Serikali hii ya awamu ya tano hatutaki kuwa na walimu wasiokuwa na sifa, bora kujiengua mwenyewe,”alisema Profesa Ndalichako.

Waziri   alisema changamoto kubwa inayoikabili wizara yake ni utekelezaji wa mipango endelevu ya wizara ambayo ni mizuri lakini utekelezaji wake ni mdogo kutokana na kuingiliana kwa mipango ya maendeleo endelevu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com