Msajili Hazina ayabana mashirika ya umma
MSAJILI wa Hazina, Lawrence Mafuru amesema kuanzia mwaka huu wa fedha, mashirika yote ya umma nchini yatatakiwa kuchapisha taarifa zao za ukaguzi wa hesabu katika magazeti ya serikali.
Aliyasema hayo mjini Dodoma jana alipozungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wakati kamati hiyo ilipopokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) za Mwaka wa Fedha 2014/15.
“Naipongeza BoT kwa kupata hati safi, ningependa mashirika yote ya umma yafikie hatua hii ya kuwa na hesabu safi, ndio maana tumeamua kuanzia mwaka huu wa fedha kila shirika lichapishe taarifa zake za ukaguzi wa hesabu hata kama lina hati chafu ili wananchi wapate taarifa,” alisisitiza Mafuru.
Alisema hatua hiyo, imelenga kuhakikisha kila shirika la umma linafanya vizuri katika kujiendesha hivyo kitendo cha ukaguzi wa hesabu zake kuwa hadharani, kitatoa motisha kwa shirika husika kufanyakazi kwa ufanisi.
Mafuru alisema endapo ukaguzi wa hesabu wa mashirika hayo utatangazwa hata mashirika yanayofanya vibaya kwa maana ya kupata hasara yataonekana, hatua itakayoibua changamoto ya kujiimarisha zaidi kwa mashirika hayo.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya mwaka ya ukaguzi wa hesabu zinazoishia mwaka wa fedha Juni 2015/16 kati ya Februari au Machi mwaka huu, hivyo kila taasisi za umma zitaanza kuchapisha taarifa zake mara baada ya ripoti hiyo.
Awali, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, aliwasilisha ripoti hiyo ya ukaguzi wa hesabu za benki hiyo ambayo pamoja na kubainika kupata hati safi, bado ilikuwa na mapungufu madogo ikiwemo tatizo la kutowasilishwa vyema kwa masurufu.
Aidha, gavana huyo alielezea hatua zinazochukuliwa na benki hiyo katika kuimarisha sekta ya fedha nchini ikiwemo hatua za kuteketeza fedha zilizochakaa ambapo hadi sasa jumla ya mashine za kisasa 26 zimenunuliwa kwa ajili ya kazi hiyo na kusambazwa katika mikoa mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment