Wananchi
wa Kijiji cha Samunge, Tarafa ya Sale, Wilayani Ngorogongoro wakiwa
wamefunga barabara kuzuia msafara wa Mkuu wa Mkoa ili waweze kutatuliwa
mgogoro ardhi ya Shule ya Msingi pamoja na Zahanati ya Samunge
iliyoporwa na wavamizi.
Mkuu wa
Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(tatu kulia) akisikiliza mgogoro wa
wananchi wa Samunge baada ya wananchi hao kuzuia msafara wake.
Mtendaji
wa Kata ya Samunge Zacharia Antony (aliyeshika file) akimuonyesha Mkuu
wa Mkoa Mhe. Mrisho Gambo(tatu kulia) barua iliyoandikiwa kinyume cha
taratibu na Mkuu wa Kituo cha Polisi Loliondo kumhalalisha mvamizi
katika eneo hilo na kuwaamuru wanakijiji kuacha kutombughudi Lemindi
Njuda (Mvamizi).
Mkuu wa
Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo akienda kukagua eneo la shule ya Msingi
Samunge lililovamiwa na Bw. Lemind Njuda (hayupo pichani).
Mkuu wa Mkoa wa Arusha (pili kushoto) akionyeshwa mipaka ya eneo la Shule ya Msingi Samunge na viongozi wa kijiji cha Samunge.
Wadau wa
Habari katika picha ya pamoja na Babu wa Samunge Mchungaji Ambilikile
Mwasapila(pili kulia) maarufu kama Babu wa Kikombe.
Babu wa
Samunge Mch. Ambilikile Mwasapila (kushoto) akiwa na Nteghenjwa Hosseah
mdau wa Habari. Babu wa Samunge ni miongoni mwa wananchi waliozuia
Msafara wa Mkuu wa Mkoa.
Nteghenjwa Hosseah ,Loliondo
Migogoro
ya ardhi katika wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha juzi iliingia katika
sura mpya baada ya wananchi wa kata ya Samunge wilayani humo akiwemo
babu wa kikombe cha dawa, Mchungaji Ambilikile Mwaisapile waliandamana
na kufunga barabara na kuzuia msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho
Gambo ili watatuliwe mgogoro wa ardhi ya shule iliyoporwa na diwani
mstaafu wa kata hiyo.
Wananchi
hao wakiwa na mabango na majani mabichi walizuia msafara huo ili waweze
kusikililizwa kilio chao cha muda mrefu baada ya baraza la kata kuamuru
katika kesi yake aprill mwaka huu kuwa ardhi hiyo ni mali ya shule
lakini jeshi la polisi Ngorongoro limekuwa likimlinda na kumkingia kifua
mvamizi huyo na kukataa kutekeleza amri ya baraza la ardhi kata
iliyomtaka kuondoka katika eneo hilo la shule.
Baadhi ya
mabango hayo yalikuwa yakisomeka ” tumeporwa ardhi yetu Mkuu wa Mkoa
tusaidie” lingine likisema ”wenye fedha wamepora ardhi ya shule na
polisi inawalinda na kuwakingia kifua” na bango lingine lililosomeka
”Mkuu wa Mkoa tunaomba ushuke utusikilize viongozi wa wilaya wote
wamenunuliwa”
Kabla ya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuteremka kuwasikiliza aliteremka Mkuu wa wilaya
ya Ngorongoro Rashid Taka na Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo OCD Warioba
kwa lengo la kuwatuliza na kuwasihii kuacha mukari ili waeleza kero zao
kwa utulivu na amani bila ya vurugu zozote.
Akizungumza
kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo, Mtendaji wa kata hiyo Zakaria
Antony alisema kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 15 limeporwa na
mfanyabiashara na diwani mstaafu Lemindi Njuda ambaye amefanya kilimo
cha migomba na shughuli nyingine za kijamii.
Antony
alisema kuwa uamuzi wa kuondolewa kwa diwani huyo wa zamani katika eneo
la shule ulitolewa na baraza la ardhi kata aprill mwaka huu lakini jeshi
la polisi wilaya ya Ngorongoro limekuwa likimlinda na kugoma kutekeleza
amri baraza na badala yake limeandika barua ya kutobugudhiwa katika
shamba hilo na hatua kali zinachukuliwa kwa mwananchi atayekiuka amri
hiyo.
Mtendaji
huyo aliendelea kusema kuwa wananchi wanashindwa kufanya shughuli za
maendeleo hususani ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu kutokana na
ufinyu wa eneo la shule hivyo walimuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia mgogoro
huo ili haki iweze kutendeka kwani polisi imewekwa mfukoni na tajiri
huyo.
Naye
Mchungaji Ambilikile Mwaisapile alisema kuwa yeye yuko mstari wa mbele
kuhakikisha shule inarudishiwa eneo lake lililoporwa na watu wenye fedha
na nguvu za ushawishi kwani mungu hapendi vitu vya dhuruma.
Mchungaji
alisema yeye pamoja na wananchi wa kata hiyo walikuwa wakisaka haki
kila ofisi ya wilaya ya Ngorongoro lakini haki hiyo walishindwa kuipata
kutokana na mapokezi mabovu ya viongozi wa serikari wilaya ya
Ngorongoro.
Mkuu wa
Mkoa Gambo kwa alimwamurisha OCD kufuta nakala ya barua aliyoandika mkuu
wake wa kituo cha polisi Loliondo kwani yeye hana mamlaka ya kufanya
hivyo bali anapaswa kutekeleza amri ya mahakama ya baraza la kata na sio
vinginevyo.
Gambo pia
alimwagiza Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro pamoja na kamati yake ya ulinzi
na usalama kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa amri hiyo
ili shughuli za maendeleo ya shule hiyo ziweze kufanyika mara moja.
Alisema
na kusikitishwa kuona wananchi wana kero ya kutaka maendeleo lakini
viongozi wa serikali kwa kujali matumbo yao na kuendekeza rushwa wako
mstari wa mbele kuzuia wananchi kufanya shughuli za ujenzi wa shule.
Pia Mkuu
huyo aliwataka viongozi wa wilaya kumaliza mgogoro mwingine wa ardhi
uliopo karibu na zahanati ya kata hiyo ili wananchi waweze kufanya
shughuli nyingine za maendeleo na kuacha kukesha kufikiria migogoro ya
ardhi kila kukicha ambayo mingi inasababishwa na viongozi.
0 comments:
Post a Comment