METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 5, 2016

CHADEMA Wazua Balaa Umeya wa Kinondoni


Wakati mchakato wa uchaguzi wa meya na naibu wake ukiendelea, suala la idadi ya madiwani wa viti maalumu wa Chadema katika Manispaa ya Kinondoni limeibua mvutano mpya kati ya chama hicho na ofisi ya mkurugenzi mtendaji.
Mvutano huo umejitokeza baada ya Mkurugenzi wa Kinondoni, Aron Kagurumjuli kutoa barua inayoeleza kuwa kutakuwa na madiwani viti maalumu wanawake wasiopungua theluthi moja ya madiwani wa kuchaguliwa wa Chadema. 
Kwa mantiki hiyo, Chadema ambayo ina madiwani wa kuchaguliwa saba itakuwa na madiwani watatu wa viti maalumu. Kwa hiyo majina yasiyopungua matatu ndiyo yatakayowasilishwa kuunda baraza jipya la madiwani.

Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo alipinga maelezo hayo ya mkurugenzi akisema: “Tayari nimeshamwandikia barua mkurugenzi kumweleza. Tungekuwa tunatoka katika uchaguzi mkuu ningekubaliana na hoja ya Kagurumjuli, lakini kwa hali ilivyo sasa siwezi kukubaliana naye kwa sababu baraza likiitishwa madiwani hawatakula kiapo kama awali.”

Kuhusu madai hayo Kagurumjuli alisema: “Nasimamia sheria, sifuati matakwa ya mtu. Nadhani wao wanapingana na sheria. Sielewi presha inatoka wapi. Wa kushinda atashinda na wa kukosa atakosa kulingana na idadi ya wajumbe wake na hakuna atakayeonewa.”

Alisisitiza kuwa kulingana na sheria hiyo na idadi ya madiwani wa kuchaguliwa wa Chadema, chama hicho hakiruhusiwi kuongeza diwani mwingine. Kagurumjuli hakuwa tayari kutaja idadi ya wajumbe watakaounda baraza la madiwani na kusema kwamba anasubiri majina ya madiwani kutoka CUF, Chadema na CCM.

Lakini Kilewo alisema msimamo wa Chadema uko palepale wa kuhakikisha madiwani wanne wanabaki Kinondoni na kwamba hakuna mwenye mamlaka ya kuengua mjumbe isipokuwa kifo na mahakama.

“Ubungo hakuna tatizo. Ingawa maelezo yanafanana ya wajumbe watatu kutakiwa kulingana na idadi ya madiwani wa kuchaguliwa. Ishu ipo Kinondoni kwa sababu madiwani wetu wa viti maalumu wengi walikubaliwa,” alisema Kilewo.

Kuhusu umeya baada ya manispaa hizo kugawanywa, Kilewo alisema jina la Mustafa Muro, Diwani wa Kinondoni, ndilo lililopendekezwa na kupelekwa kwa ajili ya kugombea umeya wa Kinondoni huku Boniface Jacob akiteuliwa kugombea Ubungo.

Wakati Kilewo akisema hayo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge alisema mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya umeya na naibu meya katika manispaa hizo ulitarajiwa kukamilika jana jioni.

“Mchakato huu ulianza muda mrefu lakini leo (jana), jioni ndiyo kilele chake. Wagombea watakaopatikana ni mahiri na CCM ipo fiti tunasubiri mechi uwanjani,” alisema Madenge.

Kwa nyakati tofauti, Manispaa za Kinondoni na Temeke zilifanya mgawanyo wa madiwani baada ya Serikali kuzigawanya na kuunda halmashauri za Ubungo na Kigamboni.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com