MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amepongeza
ukaguzi wa vyeti pamoja na mfumo wa uchumi, unaofanywa na Serikali ya
Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli.
Alisema kuwa ni hatua nzuri ya kurejesha nidhamu na maendeleo ya nchi na kuwataka wananchi kumuunga mkono na sio kulalamika.
Butiku alisema hayo juzi kwenye mazungumzo maalumu na gazeti hili,
ambapo alisema kuwa kinachoendelea kwa sasa ni utekelezaji wa sheria na
kanuni ambazo awali zilichezewa.
Alisema kushindwa kufuatwa kwa taratibu kulitengeneza mianya
mbalimbali kwa wananchi kujiamulia mambo yao, huku wengine wakiichezea
elimu ambayo ndio msingi wa taifa.
Butiku alionesha kukerwa zaidi na utitiri wa vyeti vya kufoji,
uliokuwa umekithiri serikalini na kuipongeza serikali kwa uamuzi wake wa
kukabiliana na hali hiyo sasa, kwa kufanya uhakiki wa vyeti vya
watumishi wa umma.
Alisema kuwa inashangaza kuona kuwa kuna watu walikuwa wamefikia hadi
hatua ya kuwa na vyeti vya juu vya Shahada ya Uzamili (Masters) na
Uzamivu (PHD), lakini vya kidato cha nne hawana.
“Kile kinachoendelea kwa sasa ni utekelezaji wa ahadi ya kurejesha
mifumo ya nidhamu kwenye serikali, sasa kinachotakiwa ni kuunga mkono
kwa kuhakikisha kuwa malengo ya Rais yanatimia kwa sasa,” alisema
Butiku.
Alisema anashangazwa kwa uwepo wa wanafunzi hewa katika ngazi ya vyuo
na hasa vyuo vikuu, kwa kusema kuwa hiyo ni ishara ya ukosefu wa
umakini katika elimu.
“Mimi nikitoa mfano wa miaka yetu wakati tunasoma, ni matokeo yetu
mazuri tu ndio yaliyokuwa yakitubeba na kuendelea zaidi ngazi za juu
hadi mimi ninafikia kusoma Chuo Kikuu cha Makerere Uganda ni matokeo
mazuri tu, lakini kuna muda hapa nchini ilikuwa fedha inaweza kukubeba,”
alisema Butiku.
Butiku ambaye aliwahi kuwa Msaidizi wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu
Julius Nyerere, aligusia kuhusu mfumo wa sasa wa kiuchumi, ambapo
alimpongeza Rais Magufuli kwa kurejesha fedha katika mfumo unaostahili.
Alisema kuwa ili uchumi uweze kusonga mbele ni dhahiri kuwa lazima
fedha ziende kwa wazalishaji, akiwa na maana ya watu ambao
wanazizungusha na kuendesha maendeleo.
Butiku alisema kuwa kwa sasa kinachofanyika ni fedha kurejea kwenye
matumizi stahiki na yenye tija kwa nchi nzima, huku akiwalaumu wale
wanaolalamika kuwa walikuwa wamezoea aina ya maisha ya matumizi na kwa
sasa wanakabwa na upangwaji wa bajeti.
Alisema hatua aliyochukua Rais Magufuli ni kuonesha umakini, hasa
anapokabiliana na vitendo vya uovu hasa rushwa na ubadhirifu na kuwa
hiyo inasaidia kurejesha heshima ya kimamlaka. Butiku alimtaka kutumia
fedha zaidi katika kuimarisha mifumo ya elimu na hasa kuwasomesha vizuri
vijana ili watumie elimu yao kwa tija ya taifa.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuwa
ikishughulikia kwa kina suala la elimu kwa kuendesha misako ya kubaini
watumishi hewa serikalini, pamoja na kukabiliana na matumizi mabaya ya
fedha, ambapo ni pamoja na kuzuia matumizi yasiyokuwa ya lazima hasa kwa
watendaji wa serikali.
Saturday, October 22, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
Wafanyakazi wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, wakiwa wamejipanga tayari kwa maandamano katika maadhimisho ya S...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akifurahia jambo pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment