Watu
472 waliohukumiwa adhabu ya kifo kutokana na makosa mbalimbali,
wanasubiri saini ya Rais Dk. John Magufuli ili kujua hatima ya
utekelezaji wa adhabu zao ama laa.
Taarifa
hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu adhabu ya kifo.
Bisimba alisema, watu hao walihukumiwa adhabu ya kifo kutokana na kutiwa hatiani na makakama kwa makosa ya uhaini na mauji.
Licha
ya adhabu hiyo alisema hatua ya utekelezaji wake inakwenda kinyume na
haki za binadamu kama inavyotafsiriwa katika matamko na mikataba
mbalimbali ya kimataifa.
Kutokana
na hali hiyo, Dk. Kijo-Bisimba, alisema hadi kufikia Desemba mwaka
jana, jumla ya watu 472 walikuwa wamehukumiwa adhabu hiyo.
Alisema
wakati watu hao wakisubiri adhabu hiyo, wengine 244 waliopo katika
magereza mbalimbali bado wanasubiria maamuzi ya rufaa zao.
“Licha
ya adhabu hii kutotekelezwa hapa nchini kwa takriban miaka 22 na miaka
24 ya kwanza ya uhuru, taarifa zinaonesha kuwa hadi sasa ni watu 72 tu
ambao wameshanyongwa kutokana na adhabu hiyo,” alisema.
Dk.
Kijo-Bisimba alitoa taarifa hiyo katika kipindi cha kuelekea
maadhimisho ya siku ya kupinga adhabu ya vifo duniani, ambayo itafanyika
katika nchi 70 na kaulimbiu ikiwa ni “Kuua ni Nyenzo ya Kigaidi, Acha
Mnyororo wa Kigaidi,”.
“Leo
ni miaka 14 tangu wanaharakati walivyoamua kuwepo kwa siku hii
tusipokuwa na uhai hatuwezi kufanya kitu chochote hivyo adhabu hii haina
maana kwani inaingilia haki ya uhai wa binadamu na kuona si kitu cha
thamani,” alisema Bisimba.
Mkurugenzi
huyo alisema, hadi sasa nchi 140 duniani zimeshafuta adhabu hiyo,
ambapo kwa upande wa Afrika nchi 17 zimeshakubali kufuta adhabu hiyo.
Hata
hivyo alisema ni wakati mwafaka kwa Serikali kuondoa adhabu hiyo, ili
Tanzania iwe nchi ya 18 katika bara la Afrika kufuta adhabu hiyo, ambayo
haina faida yoyote.
Mkurugenzi
huyo wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, alisema kuwa adhabu hiyo
inakabiliwa na upungufu mkubwa ikiwamo kuwapa marais ugumu kuweka saini
kwa mtu kuuawa.
“Ni
miaka 22 sasa nchi yetu haijawahi kutekeleza adhabu hiyo kwani Rais
ndiye anayeruhusiwa kwa mujibu wa sheria lakini hata wao wanaogopa
kufanya hivyo ili mtu mwingine afe badala yake wangetoa adhabu mbadala
kwani wengine wanaofanya makosa hayo ni vichaa,” alisema.
Alisema
adhabu hiyo ni ya kibaguzi na huwatia hatiani watu maskini wasiokuwa na
uwezo wa kujitetea mahakamani au kuweka mawakili.
Dk.
Bisimba, ameiomba Serikali isitunge tena sheria ya kifo na ikiwezekana
ya sasa ikiwemo iliyoongezwa ya makosa ya ugaidi iondolewe na kutafutwa
adhabu mbadala kwa mtu atakayetiwa hatiani.
“Adhabu
ya kifo imeainishwa kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16
‘Penal Code’ ambayo ililetwa na utawala wa kikoloni mwaka 1945. Hata
baada ya Uhuru 1961 hukumu ya kifo imeendelea kuwa sehemu ya sheria
licha ya marekebisho mbalimbali ya sheria hiyo ikiwemo marekebisho ya
mwaka 2002.
“Adhabu
ya kifo hutolewa kwenye makosa ya mauaji chini ya sheria hiyo kifungu
197 na kwenye hati ya kosa la uhaini chini ya kifungu cha 39 (3) (C).
“Pamoja
na hayo mwaka huu Serikali imeongeza adhabu ya kifo kama mtu akikutwa
na kosa la ugaidi chini ya sheria ya kudhibiti ugaidi ya mwaka 2002
kwenye mabadiliko madogo ya sheria, hii imeengeza makosa ambayo mtu
anaweza kuhukumiwa kifo kufikia makosa matatu,” alisema Dk. Bisimba
Alisema
kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na mikataba mbalimbali ya
kikanda na kimataifa ya haki za binadamu, zipo sababu za msingi za
kupinga adhabu ya kifo.
“Tunapenda
kuweka wazi kuwa hatufurahii watu kuua watu wengine na ndiyo maana
hatungependa hata muuaji auawe kwa vile ni sawa na kumkubalia kuua.
Adhabu ya kifo ni ya kinyama na isiyo na staha, inayotweza utu wa
ubinadamu na hufanya Serikali ionekane pia kama mhalifu kwa kuua.
“Adhabu
hii ikitolewa kwa mtu asiye na hatia kimakosa huwezi kuirekebisha kwani
mfumo wa utoaji haki huwa pia na mianya ya makosa na hivyo maisha ya
mtu yanweza kupotea bure na hakuna ushahidi kama adhabu hii inazuia watu
wengine kutotenda makosa kama hayo,” alisema
Mbali
na maadhimisho hayo kituo hicho kilizindua kitabu kinachoelezea adhabu
ya kifo na ukiukwaji wa Haki za Binadamu cha mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment