WAZIRI
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu
amesema utafiti unaonesha kuwa kwa kila watu wanne duniani, mmoja ana
matatizo ya afya ya akili.
Alisema
hayo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani
yaliyofanyika kitaifa Dar es Salaam chini ya kaulimbiu: “Utu katika Afya
ya Akili, Huduma za Kisaikolojia na Afya ya Akili kuwa Huduma ya Kwanza
kwa Wote”.
Kwa
mujibu wa Waziri Ummy wananchi wanapaswa kuwa makini kuchunguza afya
zao za akili kwa sababu utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO)
zinaashiria kuwa jamii kwa sasa inakumbwa na maradhi mengi ya namna
hiyo.
“Takwimu
kwamba kila watu wanne, mmoja wao ana ugonjwa wa akili ni kielelezo
tosha kwamba ipo haja ya jamii kujitambua na kuona umuhimu wa kupewa
elimu ya afya ya akili na kisaikolojia,” alisema na kufafanua:
“Magonjwa
ya akili ni yanayoathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na
kutenda, hivyo kuwa na tabia au mwenendo ulio tofauti au usioendana na
jamii husika kiimani, kimila, desturi na nyanja nyingine za kijamii.”
Aliongeza: “Tunapaswa
kukumbuka kuwa hakuna afya njema ya kimwili kama hakuna afya ya akili;
na pia nchi yetu ikiwa na wananchi wenye afya bora ya akili ni hazina
kubwa kwa Taifa.”
Ummy alibainisha: “Miongoni
mwa watu wanaopata matatizo ya kiakili ni wachache tu ambao wanaweza
kufikia na kupata huduma ya afya ya akili, hata hao wanaohudhuria vituo
vya afya, ni wachache wamekuwa wakipata huduma stahiki.
“Katika
nchi yetu tumekuwa tukikabiliwa na matatizo kama hayo kutokana na
ufinyu wa bajeti, ukosefu wa wataalamu katika vituo vya kutolea huduma,
ukosefu wa vifaatiba na dawa kwa wagonjwa wenye matatizo ya akili,
kijamii na kisaikolojia.”
Waziri Ummy alisema hali hiyo inatokana na matatizo yanayoikabili jamii yakiwamo majanga yanayoiandama dunia.
Mwalimu
alitoa mfano kwamba, mwaka jana Tanzania ilionesha kuwa na wagonjwa wa
afya ya akili 311,789 kulingana na takwimu za waliokwenda hospitali
kuchunguzwa.
Alibainisha
kwamba hali hiyo inaashiria kuwa idadi hiyo ni kubwa zaidi, kwa sababu
kuna ambao wana matatizo hayo lakini hawaendi hospitali au wamekuwa
wakienda kupata huduma tofauti.
Alisisitiza kuwa katika kukabaliana na ukweli huo, jitihada zimefanywa na serikali kutoa huduma za afya ya akili na saikolojia.
Mwalimu
alisema Serikali itaendelea kuongeza juhudi katika kutoa huduma na
elimu ya afya ya akili kuanzia ngazi ya msingi na kuwa na kitengo
maalumu kinachotoa huduma hizo katika hospitali zote nchini.
Hatua nyingine alisema ni kuboresha upatikanaji wa dawa za kutibu magonjwa ya akili katika hospitali zote za Serikali.
Aliongeza
kuwa Serikali imeimarisha matibabu ya akili na saikolojia katika
hospitali za mikoa na rufaa hii ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa
afya ya akili wakiwamo madaktari bingwa na wauguzi ili kuboresha huduma
kwa wagonjwa wa nje na waliolazwa.
Alifafanua
kuwa sababu za kijamii zinazoweza kusababisha mtu kupata magonjwa ya
akili ni umasikini uliokithiri, kutengwa na kubaguliwa na jamii. Sababu
zingine alizitaja kuwa ni kunyanyaswa kimwili na kingono, kuwa tegemezi,
kupoteza mali, kazi, ulevi, kukosa huduma muhimu na unyanyapaa.
Aliiasa
jamii kuachana na Imani potofu kuwa chanzo cha ukichaa ni ushirikina na
hivyo kupoteza fedha na mali nyingi kwa waganga wa kienyeji wasio
waaminifu.
0 comments:
Post a Comment