Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi.
Ripoti ya
mwenendo wa mpira wa miguu Tanzania na mipango yake inayofanywa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemfurahisha Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye hivyo moja kwa moja
akaupongeza uongozi wa Rais Jamal Malinzi akisema unafanya kazi kubwa.
Serengeti
Boys inawania kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri
katika fainali zitakazofanyika Antananarivo, Madagascar sawa na timu ya
taifa ya soka la ufukweni ambayo inatarajiwa kusafiri kwenda Abidjan,
Ivory Coast kucheza mchezo wa pili wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika kwa mchezo huo.
Timu
nyingine ya taifa ni ile ya wanawake ya Tanzania Bara maaarufu kwa jina
la ‘Kilimanjaro Queens’ ambayo kwa sasa iko Uganda kuwania taji la
Chalenji ikishirikisha timu za taifa za Afrika Mashariki katika michuano
ya inayotarajiwa kufanyika jijini Jinja kwa siku tisa kuanzia Septemba
11, mwaka huu.
Nape
amefurahishwa na mipango ya TFF baada ya kupeleka timu zote kushiriki
michuano mbalimbali kwa vipindi mbalimbali na kwamba Serikali itasapoti
lakini hapo baadaye baada ya kufuata taratibu mbalimbali baada ya Rais
Malinzi kumfafanualia kuwa gharama za kuendesha mpira kwa mwaka zinafika
shilingi bilioni 15, na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) huchangia asilimia tatu (3) tu ya bajeti nzima kwa mwaka.
“Kwa
kuanzia msimu huu tu, FIFA imeongeza na sasa itafika asilimia 6 kwa
mwaka,” alisema Malinzi jambo ambalo lilimshangaza Nape ambaye leo
Septemba 10, 2016 alifanya ziara ya kutembelea TFF kujionea hali halisi
na kushangazwa na taarifa za vyanzo mbalimbali zinazotuhumu shirikisho.
Nape alisema: “Serikali inasapoti maendeleo, lakini lazima yafuate taratibu, kanuni na sheria za soka.”
Katika
eneo la kufuata taratibu, kanuni na sheria za soka hatua nyingine, Nape
alitaka Malinzi na kamati zake kuwa wakali kwa kuwa huwa hawachui hatua
mapema, inatokea wadau kutaka kuipanda kichwani TFF.
“Naagiza
mchukue hatua mapema kukamua majipu kabla hajajaiva. Sasa ninyi
mnasubiri kwa muda mrefu kabla ya kuchukua hatua, ndiyo maana
wanawasumbua. Washughulikieni mapema, mkiwabana mapema watakaa kimya,
kanuni mnazo, sheria mnazo, wabaneni,” alisema Nape.
Katika
hatua nyingine, Nape alisema kwamba kuna mchakato unaendelea kwa sasa
ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kwamba wanarejesha
mamlaka ya kumiliki baadhi ya viwanja vya soka Makao Makuu ya chama
badala mikoa ambako wamegundua kuwa kuna matatizo makubwa katika
menejimenti.
NA HIZI
NDIZO SALAMU ZA RAIS WA TFF, JAMAL EMIL MALINZI KWA MHESHIMIWA NAPE
NNAUYE WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO UWANJA WA KARUME
TAREHE 10 SEPTEMBA 2016
Mheshimiwa Waziri,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutukutanisha hapa leo.
Ni jambo
la heshima na furaha kubwa sana kwetu sisi wanafamilia ya mpira wa
miguu Tanzania kwa kutembelewa na wewe Mheshimiwa Waziri na ujumbe wako.
Mheshimiwa ahsante sana kwa tukio hili adhimu na karibu sana kwenye
makazi ya mpira “home of football”.
Mheshimiwa
Waziri tunashukuru kwamba umeweza kutembelea eneo letu na kujionea wapi
huwa tunafanyia shughuli zetu mbali mbali za kuendeleza michezo.
Shirikisho
la mpira wa miguu Tanzania TFF limesajiliwa chini ya sheria ya baraza
ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 1971 na madhumuni yake
makuu ni kuendeleza na kusimamia mpira wa miguu Tanzania. Katika
kutekeleza azma hii shughuli zetu tumezigawanya katika maeneo makuu
matano:
- Utawala
Shughuli
za kila siku za uendeshaji wa mpira wetu zinasimamiwa na Sekretariet ya
TFF inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndugu Mwesigwa Selestine. Chini yake ana
vitengo vikuu vitano: Ufundi ambacho kinasimamia maendeleo ya mpira,
Mashindano ambacho kinasimamia mashindano mbali mbali, Fedha na utawala,
Sheria na vyama wanachama na cha tano ni cha biashara na masoko.
Vitengo hivi kwa pamoja vinashirikiana kuhakikisha mpira unafundishwa,
unachezwa na unasimamiwa vyema. Aidha zipo Kamati mbali mbali
zinazotusaidia kutushauri kwenye mambo ya kitaalam na kutoa maamuzi
vikiwa vyombo huru. Pia tunacho chombo chetu kinachoitwa Bodi ya Ligi
kinachosimamia uendeshaji wa ligi zetu kuu tatu Ligi kuu ya daraja la
kwanza na ya daraja la pili. Ligi kuu ya vilabu vya wanawake
inaendeshwa na kamati ya mpira wa wanawake.
- Mashindano
Ili mpira
uchezwe inabidi kuwepo na mashindano. Wakati wote TFF inafanya jitihada
za kubuni mashindano mapya na kuhakikisha yaliyopo yanafanyika kwa
mujibu wa kalenda. Kwa sasa TFF tunaendesha mashindano makuu ya kitaifa
saba: Ligi kuu, Ligi daraja la kwanza, Ligi daraja la pili, Ligi ya
mikoa, Kombe la Shirikisho, Ligi ya vijana na Ligi ya vilabu vya
wanawake. Ukiondoa ligi daraja la pili na ligi ya mikoa mashindano
yaliyobakia yote yanaonekana moja kwa moja kwenye (live) kwenye
Televisheni. Shirikisho liko mbioni kuanzisha mashindano ya vilabu nane
bora vya ligi kuu (Super 8). TFF pia huwa inasimamia mechi mbali mbali
za kimataifa za mashindano na za kirafiki kwa timu za Taifa za rika
mbali mbali za wanawake na wanaume.
- Masoko na Biashara
Kuendesha
mpira ni gharama kubwa. Wastani wa bajeti ya Shirikisho ni shilingi
bilioni kumi na tano kwa mwaka.Tunawashukuru FIFA ambao hadi mwaka jana
walikuwa wanachangia asilimia 3% ya bajeti hii na kuanzia mwaka huu
wanachangia asilimi 6% ya bajeti hii. Jitihada kubwa zimekuwa
zikifanyika kuhakikisha shughuli za uendeshaji wa mpira hazikwamishwi na
ukosefu wa fedha. Kitengo cha biashara na masoko kinafanya jitihada
kubwa kuhakikisha kila shindano letu linakuwa na udhamini hata kama sio
wa kukidhi mahitaji yote.
- Miundombinu
Ni muhimu
sana kuwa na miundo mbinu ya kutosha na yenye sifa ya kuchezewa mpira.
Kwa kushirikiana na wamiliki mbali mbali wa viwanja vya mpira TFF
tumekuwa tukitoa ushauri wa namna ya kuendeleza na kutunza viwanja vyetu
vya mpira ili vifae kuchezewa mpira wa kisasa. Aidha tunashukuru
Halmashauri ya jiji la Tanga kwa kuiipatia TFF miliki ya eneo la ekari
18 jijini Tanga, kwa kushirikiana na FIFA eneo hilo litajengwa kituo cha
kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira cha TFF. Michoro yake iko katika
hatua za mwisho za maandalizi.
- Maendeleo ya mpira wa miguu.
TFF
tumejiwekea malengo mawili makuu: Kucheza fainali za dunia mpira wa
miguu wa wanawake Paris mwaka 2019 na kucheza fainali za kombe la dunia
wanaume mwaka 2026.
Kwa
upande wa mpira wa wanawake katika kufikia azma hii mwaka huu
tunaanzisha ligi kuu ya vilabu vya mpira wa wanawake (Tanzania Women
Premier League). Kutokana na ligi hii vipaji vitaibuliwa kwa ajili ya
kuimarisha kikosi cha timu yetu ya Taifa Twiga stars. Kikosi hiki
mwakani kitakuwa kikikusanywa mara kwa mara, kufanya mazoezi na kucheza
mechi za kirafiki za kimataifa ili kujiandaa na hatua za awali za kombe
la dunia mwaka 2018.
Kwa
upande wa maandalizi ya Taifa stars kuelekea mwaka 2026 tayari program
yetu imeanza kwa kuwa na Serengeti Boys ambayo inapambana kucheza
fainali za vijana za Afrika mwakani umri chini ya miaka 17. Kwa sasa
kikosi hiki kiko kambini Seychelles kujiandaa na mechi dhidi ya Kongo
tarehe 18 Septemba . Timu hii pia ndiyo itapambana kucheza fainali za
Afrika za vijana umri chini ya miaka 20 mwaka 2019. Aidha kwenye shule
ya Alliance huko Mwanza tayari tuna kikosi cha awali cha timu ya Taifa
cha vijana umri chini ya miaka 15 ambacho kinaandaliwa kucheza fainali
za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tanzania tutakuwa wenyeji
wa fainali hizi kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu.
Pia mwaka
huu tunaanzisha ligi ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 20.
Kutokana na ligi hii mwakani itaundwa timu ya Taifa ya awali ya vijana
umri chini ya miaka 23 itakayopambana mwaka 2019 kutafuta fursa ya
kucheza fainali za Olimpiki Tokyo mwaka 2020. Kutokana na makundi haya
makuu matatu kuanzia mwaka 2021 walimu wetu wa mpira wataweza kuanza
kutengeneza kikosi imara cha Taifa stars kuelekea Fainali za Kombe la
dunia 2026. Gharama kubwa zinahitajika kugharimia program hizi na
tunaomba Serikali na wadau wengine mtushike mkono ili tufikie azma yetu
ya kucheza World Cup 2026.
Mheshimiwa
Waziri ninaomba nigusie uendeshaji wa ligi yetu kuu na utoaji wa leseni
za vilabu.Kama nilivyosema hapo awali Ligi kuu inasimamiwa na bodi ya
ligi kwa maelekezo ya kanuni za mashindano kama zinavyopitishwa na
kamati ya Utendaji kila mwaka. Mheshimiwa Waziri kinacholiongoza
Shirikisho katika uendeshaji wa ligi kuanzia usajili, upangaji wa
ratiba,upangaji wa waamuzi na utoaji wa adhabu ni kwa mujibu wa kanuni
tulizojiwekea na kauli mbiu ya #fairplay,haki mchezoni.
Ninaomba
nieleze pia kuwa kufuatia maagizo ya FIFA sasa tupo hatua za awali za
kutoa leseni kwa vilabu zinazohalalisha vilabu kushiriki katika ligi.
Mahitaji makuu ya leseni hizi ni klabu kuwa na menejimenti na kumbukumbu
za mahesabu yake ya fedha ,kuwa na maeneo ya kufanyia mazoezi na
kucheza mechi,kuwa na program za maendeleo ya mpira wa vijana na mwisho
kueleza kinagaubaga nani anamiliki na kuendesha shughuli za kila siku za
za klabu (ownership and control). Katika hili la umiliki ni marufuku
klabu zaidi ya moja katika ligi moja kumilikiwa na mtu au mamlaka moja.
Pia kanuni ya leseni za vilabu ina kipengele cha kipimo cha sifa cha
nani anaruhusiwa kumiliki au kuendesha klabu ya mpira wa miguu , mipaka
ya mamlaka yake na mahusiano na Shirikisho na mamlaka nyingine za juu
zikiwemo Serikali,FIFA,CAF na CECAFA.
0 comments:
Post a Comment