Ndugu zangu,
Kama
uchumi wa nchi unakua, ni tafsiri ya nchi husika kuweza kutumia
rasilimali zilizopatikana kwenye kuwekeza kwenye maeneo makuu, kwa nchi
kama yetu ni Elimu na Afya ya wananchi, ambao sio tu wenye kustahili
kunufaika na kukua huko kwa uchumi, bali pia ni walio muhimu
tunapotafakari hatua ya pili ya nchi kukua kiuchumi.
Kama
nchi, lengo letu kuu ni maendeleo. Hivyo, tunapaswa kuangazia ustawi wa
wananchi na hivyo basi, kuwaangalia wananchi kama rasilimali watu kwa
maendeleo ya nchi.
Shida ni
pale dhana ya Maendeleo inapochanganywa na dhana ya ukuaji wa uchumi kwa
nchi. Hapo tunaanza kuona ukuaji wa uchumi kama LENGO la Maendeleo.
Yumkini kukua kwa pato la taifa ni kitu kimoja na Maendeleo ya Taifa ni
kitu kingine.
Na
tunapoanza kufikiri kuwa Maendeleo ya taifa ni sawa na kukua kwa pato la
taifa, ndipo hapo tunapoanza kumulikia kwenye vipimo vyenye kutuonyesha
kwamba nchi ni tajiri. Hivyo, chochote kile kinachopelekea kwenye
kupatikana kwa fedha ndicho kinachoonekana chenye kuinua maendeleo ya
taifa.
Kwa sasa
hali ya uchumi wa dunia kwa ujumla wake si njema. Tanzania si kisiwa.
Hatuwezi kujitenga na tukaendelea. Ili tupige hatua kiuchumi tunategemea
pia ustawi wa afya ya uchumi wa dunia. Tunahitaji kuendelea kuwavutia
wawekezaji wa ndani na wa nje. Ni kwa kuwawekea mazingira rafiki ya wao
kuwekeza.
Duniani
hapa si majukumu ya Serikali kuendesha viwanda au kufanya biashara
nyingine. Jukumu kubwa la Serikali zote za dunia ni kukusanya kodi yenye
kutokana na kuandaa mazingira ya uchumi kukua kutokana na iwe viwanda,
kilimo au biashara. Kisha ni kazi ya Serikali kufanyia kazi vipaumbele
kwenye huduma kwa jamii kama vile afya na elimu.
Nchi yetu
kwa sasa haina msingi imara wa kiuchumi. Kilimo kilipaswa kiwe msingi
imara wa uchumi wetu. Kazi ya kuujenga msingi huo tulishaianza na hata
tukiamini, kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa taifa letu.
Ajabu ya
uti wa mgongo huu ni kwamba kilimo na wakulima wa nchi hii kihistoria ni
kama wamepewa mgongo na Serikali. Dhana ya Kilimo Kwanza ilipotangazwa
ilirudisha matumaini, lakini, kuna dalili za kufifia tena ili hali
Uchumi wa Viwanda ambao Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Pombe
Magufuli umedhamiria kuujenga, bila shaka, na viwanda hivyo vitahitaji
malighafi zitokanazo na kilimo. Kwa muktadha huo, hatuwezi kukikimbia
kilimo kama msingi wa uchumi wetu. Tuna lazima wa kukiimarisha na
kukienzi kilimo. Ni kutokana na ukweli pia, kuwa sekta ya kilimo ndio
yenye kuajiri asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania.
Na hata
tukitumia mfano wa kilimo hicho hicho, uchumi unahitaji uwe na mizizi
imara ili uweze kukua. Na matunda yake, mathalan elimu na afya, hayawezi
kuwa bora yakavunwa kama hatujamwagilia maji vya kutosha mche wa uchumi
na mizizi yake.
Msingi imara wa kiuchumi hupelekea sekta nyingine za maendeleo kunawiri.
Na kwa
watendaji Serikalini, mtazamo nao uanze kubadilika, kutoka kwa Serikali
kuongoza shughuli za kiuchumi kwenda kwenye kuratibu zaidi.
Kwa
uchumi kukua na maendeleo kupatikana, kunahitaji kujenga utamaduni wa
kubana matumizi na kuweka akiba ili kuwekeza tena kwa ukuaji wa uchumi
wa baadae.
Serikali
imeanza na hatua hizo, haipaswi kuishia Serikalini tu. Wananchi
wakilifanya hili kuwa ni utamaduni wao ni jambo jema. Lisiwe la
kulazimisha, taratibu watu wenyewe wataona faida zake. Maana, mfumo
tunaokwenda nao sasa umewapunguza ' wezi' wengi na hata wafanyabiashara
wababaishaji. Hata wakibaki wachache wenye kufuata taratibu hilo ni
jambo jema kwa taifa kuliko wengi wenye kutofuata taratibu ikiwamo
kukwepa kodi.
Na kuwepo
na uwiano pia wa hali ya kuchanganyikiwa kwa kasi tarajiwa ya maendeleo
ya haraka na kasi ya maamuzi ya kutekeleza yenye kuleta mabadiliko
katika jamii. Hilo la mwisho ni lenye kuhitaji busara na hekima nyingi
ya viongozi wa kisiasa na watendaji.
Kwa
kuhitimisha, umma unapaswa kuwa na uvumilivu. Maendeleo ya kiuchumu ni
mchakato. Huenda hatua kwa hatua. Matunda yake hayawezi kuonekana kwa
haraka.
Muhimu ni kujua, kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kuchukua wajibu wake.
Maggid,Iringa.
0 comments:
Post a Comment