METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 14, 2016

Serikali yatoa majibu ya hatua iliyofikia kuhusu viwanda ilivyovibinafsisha

Serikali inatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli la kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa vinafanya kazi linatekelezwa tangu mwezi Novemba mwaka 2015.
Hayo yalibanishwa jana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Mhe. Yahaya Massare lililohusu utekelezaji wa ahadi ya Rais kuvirudisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi.

Waziri Mwijage alisema kuwa Serikali kupuitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inaendelea na zoezi la kuchambua mikataba ya mauzo kwa viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo ama havifanyi vizuri au vimesimamisha uzalishaji kabisa.

Waziri alibainisha kuwa timu ya wataalamu toka Wizara ya Viwanda na Ofisi ya Usajili wa Hazina walifuatilia na kufanya tathimini kwa kutembelea kiwanda baada ya kiwanda hatua ambayo inasaidia kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopelekea kiwanda kutofanya kazi.

Aidha, Waziri Mwijage alisema kuwa uchambuzi wa mikataba ya viwanda hivyo unafanyika kwa ushirikiano na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Wizara za kisekta ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Nishati na Madini, pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Hata hivyo, Waziri Mwijage alisema kuwa katika kutekeleza ahadi hiyo ya Rais, Serikali imetwaa Kiwanda cha Chai Mponde kilichopo wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ambacho mwekezaji amekiuka makubaliano ya mkataba.

Mbali na hayo, akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Mwakasaka lililohusu mpango wa Serikali kujenga maabara ya kupima ubora na kiwango cha asali inayozalishwa hapa nchini.

Waziri Mwijage alisema kuwa Serikali inaendelea kuhimiza ujenzi wa viwanda nchini ikiwemo viwanda vya asali na kuhakikisha vinakuwa na maabara zinazoweza kupima viwango vya msingi.

Waziri Mwijage aliongeza kuwa kuhusu ujenzi wa maabara mkoani Tabora, Wizara itahakikisha wawekezaji wanaofuatilia ujenzi wa viwanda vya asali wanakuwa na maabara za kupima viwango vya msingi vya msingi na kuiachia TBS kuweka viwango vya kitaifa na kudhibiti viwango hivyo.

Na Beatrice Lyimo, MAELEZO, Dodoma
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com