METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, September 13, 2016

SERIKALI INAENDELEA KUPOKEA NA KUHAKIKI MADAI YA WATUMISHI WA UMMA YANAYOHUSU MISHAHARA


Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma13/09/2016

Serikali imeendelea kupokea na kuhakiki madai ya watumishi wa umma yanayohusu mshahara na kuyalipa kadri ya uwezo wake kifedha.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Singida Mjini Mhe. Mussa Sima lililohusu mpango wa Serikali kulipa madeni ya watumishi.

Waziri Kairuki amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali ililipa madai ya malimbikizo ya mshahara wa shilingi 56,293,372,627.37 ambapo yalilipwa kwa watumishi 55,688 waliokuwa na madai yatokanayo na kupandishwa vyeo, ajira mpya na sababu nyinginezo.

Aidha, Waziri Kairuki amesema kuwa kwa mwaka 2015/2016 Serikali imeendelea kulipa madai ya malimbikizo ya mshahara wa watumishi wa umma ambapo hadi kufika mwezi Juni, 2016 watumishi 31,032 walilipwa jumla ya shilingi 28,929,095,373.89.

Pia ameongeza kuwa madai ya mishahara ya watumishi 7,871 yenye jumla ya shilingi 13,754,462,429.29 yameshahakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kitumishi za mshahara yakisubiri kulipwa na madai ya watumishi 8,776 yanaendelea kuhakikiwa ili yaingizwe kwenye mfumo tayari kwa kulipwa.

Akijibu swali la Mhe. Zubeda Sakuru (Viti Maalum) lililohusu changamoto ya maslahi kwa watumishi wa sekta ya afya Waziri Kairuki amesema kuwa Serikali inatambua na kudhamini mchango unaotolewa na madaktari, matabibu na wauguzi nchini.

Hivyo, Serikali imeendelea na jitihada za kuboresha mishahara ya watumishi wake mwaka hadi mwaka ikiwemo ya wataalamu wa sekta hiyo kwa kuzingatia uwezo wa Serikali wa kulipa.

Waziri Kairuki amesema kuwa Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi, punde itakapokamilika itapanga mishahara na motisha upya kwa watumishi wote wa umma wakiwemo wa sekta ya afya.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi kadri ya uwezo wake wa kulipa utakavyoimarika ambapo katika shughuli za kila siku madeni huzalishwa lakini ni azma yake kuhakikisha madeni hayo yanalipwa mara yanapojitokea.

Mbali na hayo, Waziri Kairuki ametoa wito kwa wataalamu wa afya na watumishi wote kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia viapo na maadili ya kazi zao.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com