RAIS John Magufuli amezindua ndege mpya mbili za serikali zilizonunuliwa
aina ya Bombardier Dash 8 Q400 huku akiwapasha wale waliokuwa wakibeza
ununuzi wa ndege hizo, akitaka Bodi mpya ya Kampuni ya Ndege Tanzania
(ATCL) kutosita kuwafukuza kazi wafanyakazi watakaobainika kuhujumu
kampuni hiyo.Aidha, ametangaza kuwa serikali imeanza mazungumzo ya kununua ndege
nyingine mbili mpya, ikiwamo itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 240.
Kwa upande wao, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imependekeza
ndege hizo kuitwa ‘Hapa Kazi tu’ iwapo Rais ataridhia jina hilo kwani
serikali haijanunua ndege mpya tangu mwaka 1978. Ndege hizo zitakodishwa
kwa ATCL.
Uzinduzi huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (Terminal 1), Dar es Salaam, ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa serikali akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Spika wa
Bunge, Job Ndugai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Makatibu
Wakuu na Mawaziri wa wizara mbalimbali.
Rais Magufuli alisema watu wengi wamekuwa wakibeza ununuzi wa ndege hizo
zilizotengenezwa nchini Canada na wakati mwingine alifikiria kwa nini
aliamua kufanya jambo hilo; kwani wengine wamekuwa wakisema haina spidi
na wengine kuwa ni mkweche, jambo ambalo siyo la kweli na kusema watu
hao watakuwa wa kwanza kupanda kwani zinatumika na nchi nyingine kama
Marekani wanazo 40 na pia Ethiopia.
“Wengine walilalamika kwa nini tumenunua kwa fedha taslimu, sasa mtu
ukiwa tajiri kwa nini usinunue ‘cash’, kwa nini ukopeshwe ili watu
wapate faida, kuna fedha za Watanzania na wanataka ndege ndiyo maana
tukanunua ‘cash’, ” alisema Rais Magufuli.
Alisema ndege hizo ni nzuri na ukitaka kujenga uchumi wa kisasa lazima
uwe na ndege na ukitaka kuwa na watalii hakuna sababu ya kuwafanya
waende kwenye nchi nyingine ili waje nchini mwenu lazima ziwepo ndege.
Rais Magufuli alisema kwa ndege ya aina ya Jet kutoka Dar es Salaam
kwenda Songea unatumia mafuta ya Sh milioni 28.5 lakini ukitumia ndege
hizo mpya unatumia Sh milioni moja kwa umbali huo wakati kufika tofauti
yake ni dakika 20 tu.
Alisema wanaopiga vita ni wafanyabiashara, hivyo kama wanataka spidi
wakapande za jeshi ili wafike haraka wanapotaka kwani inafanyika
biashara lazima kuangalia mazingira yote na viwanja vyote kutumika.
Alisema nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ni Sh 800,000 lakini
hizi hazitafika huko na uzuri wa ndege hizo zitatua katika viwanja vya
ndege vya mazingira yote nchini.
Rais aliwaomba Watanzania kutopuuza vitu vyao na kama hataki ni kukaa
kimya na kuacha kiherehere na kuzoea kusifia wengine na kuhoji, kwa nini
wasisifie vya kwao kwani ndege hiyo itatumika na watu wa itikadi
mbalimbali kwa kuwa ni ya Watanzania.
“Ni lazima Watanzania kujifunza kujivunia vya kwao… lazima mfahamu kwa
kulipa ndege hizo polepole tungelipa gharama kubwa tofauti na
tulivyolipa fedha taslimu, tumepunguza gharama na tuna mpango wa kununua
ndege mbili kubwa na fedha zipo,” alisema.
Alieleza kuwa ndege hizo ipo itakayokuwa na uwezo wa kubeba watu 160 na
nyingine 240 na kwamba yalipofanyika majadiliano wahusika walikuwa
wanaweka muda mrefu kwa kusema ndege ya abiria 240 italetwa mwaka 2021,
lakini tunajadiliana ili kuzipata mapema na fedha zipo.
Alisema ndege hizo zikinunuliwa itaondoka Dar es Salaam mpaka Marekani,
China bila kutua na itawawezesha watalii kutoka nchini mwao na kuingia
moja kwa moja hapa nchini bila kupitia nchi nyingine. Alitaka wizara
kuendelea na mchakato kwa kuitisha kampuni ili uwepo ushindani na
kununua kwa bei nafuu kwani wananunua kwa fedha taslimu.
Alisema ndege hizo mbili mpya zilizozinduliwa jana wanazikodisha kwa
ATCL na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kutengeneza bodi
nzuri ya wasomi wakati Mkurugenzi Mkuu wa ATCL akitokea nchini Senegal
alipokuwa akifanya kazi huko hivyo mwendo wa kucheza umekwisha.
Alielezea baadhi ya vitu vilivyofanya ATCL kutofanikiwa kuwa ni pamoja
na kutokuwa na mfumo wa kujiendesha kwa kujitegemea kibiashara muda wote
kutegemea serikali, kubweteka kwa wafanyakazi wake, hujuma ya
wafanyakazi, kutengeneza hasara za ajabu ajabu, mafuta hewa kwa
kudanganya ndege imesafiri, lakini kumbe bado iko hapo hapo pamoja na
kujilipa malipo ya ziada.
Aliwaomba bodi na wizara kutokuwa na huruma kwa wasiofaa kwa kuwafukuza
kazi kwa kuchambua kweli kweli na kuwachekecha ili kupata watu wanaotaka
kubadilika na kuwaomba wafanyakazi wanaotaka kufanya kazi kweli
kujisalimisha.
“Nakueleza waziri usiogope kupunguza wafanyakazi kama tulipunguza NIDA
600 hatuwezi kushindwa hawa 200 kwa ambaye hawezi kwenda na spidi yetu
atupishe na kwenda na waliojipanga kwenda kwa spidi tunayotaka wengine
wape fedha zao wapumzike, kwani tunataka siku moja shirika hili liwe na
ndege hata 10,” alisema.
Aliomba uongozi wa ATCL kutotumia mawakala kukatisha tiketi ila
wazingatie huduma watakazotoa na huku akikosoa sare za wafanyakazi
ambazo alisema zinatia kichefuchefu na kuwataka kujipanga vizuri ili
walipakodi waone matunda yake.
Aliomba pia bodi na menejimenti kutoruhusu kiongozi wa serikali kusafiri
bure hata kama ni yeye au waziri wa wizara hiyo au bodi kwani kuna
wakati wanakuwa wanajipendekeza wakati wanatakiwa kufanya biashara.
Akizungumzia uboreshaji wa Reli ya Kati, Rais Magufuli alisema kwa sasa
ujenzi wa reli mpaka Mwanza na Isaka mpaka Burundi zabuni zimetangazwa
na fedha zipo.
Alisema kwa reli ya zamani umepatikana mkopo kutoka Benki ya Dunia na
mabehewa yameongezeka na siku zijazo Dar es Salaam itakuwa na treni ya
umeme kwani haya yanawezekana siyo Ulaya tu hata hapa nchini
yatafanyika.
Akizungumzia ununuzi wa ndege hizo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema mara ya mwisho kwa serikali
kununua ndege mpya ilikuwa 1978 na shirika lilikuwa likitumia ndege za
kukodisha na kusababisha madeni.
Akizungumzia sifa za ndege hizo mpya, alisema ni miongoni mwa ndege za
kizazi kijacho na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kutumia mafuta
kidogo huku zikitua viwanja vyote nchini vya lami na visivyokuwa na
lami.
Alisema ndege hizo kila moja ina uwezo wa kubeba mizigo tani 1.6 na
abiria 76 na kati yao sita wanabebwa katika daraja la kibiashara na
katika hatua za awali wamejipanga kutoa huduma katika viwanja 12.
Alivitaja viwanja hivyo kuwa ni Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza, Dodoma,
Arusha, Kilimanjaro, Bukoba, Kigoma, Tabora, Mbeya, Mtwara na Comoro
huku wakiendelea na upembuzi yakinifu ili kuongeza viwanja vingine ili
ndege ziweze kutua.
Alimpongeza Rais kwa uamuzi wa kununua ndege hizo na kuonesha kuwa ni
kiongozi wa vitendo kuliko maneno na wanapendekeza ndege hizo kama rais
ataridhia ziitwe ‘Hapa Kazi Tu’.
Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema uamuzi wa kununua
ndege za aina hiyo ulifanyika kwa kuzingatia sifa za kutua na kuruka
katika viwanja vya lami na visivyo na lami, kutumia mafuta kidogo kwenda
umbali mrefu hivyo gharama za uendeshaji kuwa ndogo.
Alisema ndege hizo zina uwezo wa kubeba mzigo mkubwa na injini zenye
kazi hivyo kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga na unafuu wa bei na
kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji.
Balozi Kijazi alisema ndege hizo ni za serikali na siyo za ATCL hivyo
wataingia mkataba kwa kukodisha ndege kwa kampuni hiyo na kuzilipia
hivyo lazima kampuni hiyo kujipanga kuingia katika ushindani wa usafiri
huo.
Thursday, September 29, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. ...
-
Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya kilim...
-
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa nne kushoto) akipitia taarifa ya ujenzi wa mradi wa Maji Nyamtukuza Wilayani Nyang’...
-
Na Dotto Mwaibale KUNDI la uhalifu la watoto wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 25 maarufu kama panya road linatishia usalama wa ...
-
Na Debora Charles (Mtakwimu) Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusamba...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment