Baada
ya kufanya uhakiki wa Wanafunzi Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umebaini
uwepo wa wanafunzi hewa 2331 katika shule za Sekondari za Mkoa huo.
Taarifa
hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka wakati
alipozungumza na Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata mara baada ya
kuwakabidhi Vishikwambi (Tablets) vilivyotolewa na Shirika lisilokuwa la
Kiserikali la EQUIP Tanzania kwa ajili ya utunzaji wa Takwimu muhimu za
Sekta ya Elimu.
Mtaka
amesema kati ya Halmashauri sita za Mkoa huo, Ni Halmashauri ya Wilaya
ya Bariadi tu ambayo haina wanafunzi hewa wakati Halmashauri ya Wilaya
ya Busega ikiwa na wanafunzi hewa 110, Itilima 2137, Maswa 14, Meatu
125 na Halmashauri ya Mji wa Bariadi 439.
Kufuatia
kuwepo kwa wanafunzi hewa Mkuu wa Mkoa huo amesema, Serikali Mkoani
humo imepanga kufanya mabadiliko ya Wakuu wa Shule za Sekondari katika
Mkoa mzima, wakati taratibu za kinidhamu zikiendelea kwa wakuu wa shule
waliotoa takwimu za uongo za wanafunzi katika shule zao, wakati kwa
upande wa shule za Msingi, mabadiliko yatafanyika baada ya kumaliza
mtihani wa darasa la saba.
Mtaka
amesema kabla ya uteuzi wa wakuu wa shule na walimu wakuu utafanyika
upekuzi (vetting) kwa wale watakaopendekezwa ili kujiridhisha kama
wahusika wana sifa na uwezo wa kuendesha shule na kusimamia fedha za
Serikali zinazopelekwa shuleni kwa ajili ya kugharama elimu ya bila
malipo.
“
Serikali inaendelea kupelekea fedha moja kwa moja katika akaunti za
shule, kwa hiyo mkuu wa shule au mwalimu mkuu ni afisa masuuli katika
shule yake. Ipo haja kwa sisi kujiridhisha kama Serikali kuwa
anayeteuliwa kushika nafasi ya kuongoza shule ana uwezo na sifa ya
uadilifu. Sitakuwa tayari kuona katika mkoa huu kuna walimu wakuu
wazoefu wa kula fedha za Serikali na wakaendelea kuongoza shule” alisema Mtaka.
Akitoa
shukrani kwa Shirika la EQUIP Tanzania, Mkuu wa Mkoa amesema Shirika
hilo limekuwa msaada katika kutatua baadhi ya changamoto za Watendaji
katika Sekta ya Elimu mkoani Simiyu ikwa ni pamoja na kuwawezesha
Waratibu Elimu Kata kwa kuwapa pikipiki na kuwapa fedha za mafuta
shilingi 206,000 kwa kila mwezi pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wakuu
na walimu wakuu wasaidizi.
Aidha,
Mtaka amesema analishukuru shirika hilo kuona umuhimu wa kutoa
vishikwambi kwa Walimu wakuu na Waratibu Elimu Kata ambavyo ameelekeza
vitumike kutunza takwimu sahihi za kieleimu ikiwemo idadi ya walimu na
wanafunzi.
Kwa
upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amewataka
Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata kuvitunza vishikwambi hivyo na
kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Naye
Mkuu wa EQUIP Tanzania Mkoa wa Simiyu, Phoebe Okeyo amesema Vishikwambi
hivyo vitawasaidia Viongozi wa Elimu ngazi ya Mkoa, Wilaya na kata
kupata taarifa za masuala mbalimbali yanayofanyika shuleni.
“Sasa
hivi mtegemee kupata taarifa sahihi katika sekta ya Elimu kwa sababu ya
hivi vifaa tulivyovitoa leo, tumeanza kama pilot study kwa Mikoa ya
Simiyu, Shinyanga, Mara, Tabora, Dodoma,Lindi na Kigoma. Tunatarajia
kuongeza mikoa ya Katavi na Singida Januari, 2017” alisema Okeyo.
Jumla
ya Vishikwambi(tablets) 637 vimetolewa kwa Walimu wakuu 516 na
Waratibu Elimu Kata 121 kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu,
ambapo kila kimoja kina thamani ya shilingi 315,000/=.
0 comments:
Post a Comment