METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, August 20, 2016

SERIKALI KUNUNUA RADA SITA ZA KISASA

REIA1
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ally Karume mara baada ya kumtembelea ofisini kwake Kisiwani Unguja.
RIA2
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa wakati viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Kisiwani Unguja. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ally Karume.
RIA5
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ally (kulia) Karume wakati alipotembelea taasisi zilizochini ya Wizara hiyo. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hiyo Mustafa Abood Jumbe.

RIA6
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mustapha Abood Jumbe afafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati)   katika kikao kazi mjini Unguja.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kutangaza zabuni kwa ajili ya ununuzi wa rada sita za kisasa kwa ajili ya kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa safari za anga hapa nchini.

Prof. Mbarawa amesema hayo mjini Unguja mara baada ya kukagua shughuli zinazofanywa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Uwanja wa Ndege wa Zanzibar ambapo amesisitiza umuhimu wa kufata sheria katika kumpata mzabuni.

“Tumejipanga kuhakikisha kwamba miundombinu ya safari za anga nchini inaimarika ili kuvutia utalii na usalama wa abiria wa usafiri wa anga”, amesema Prof. Mbarawa.

Ameitaka TCAA kuhakikisha kwamba marubani wanaopewa vibali vya kurusha ndege nchini wanakidhi vigezo vya kimataifa ili kuufanya usafiri wa anga kuwa salama na wa uhakika.

Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ally Karume amempongeza Prof. Mbarawa kwa ushirikiano anaoufanya kati ya Wizara hizo na kusisitiza kuwa hali hiyo itaongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli za Serikali na kuleta tija kwa wananchi.

“Huduma wanazozipata bara ni vyema na sisi Zanzibar tukanufaika nazo ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano ili kuleta usawa kwa wananchi wa pande zote za Muungano”, amesisitiza Balozi Karume.

Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa amezungumzia umuhimu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kubadilisha mfumo wa masafa wa 700MHZ kutoka kwenye analogia kwenda Digitali ili kuuwiana na upande wa Tanzania Bara na hivyo kuondoa muingiliano wa mawasiliano.

Profesa Mbarawa yupo Mjini Unguja katika ziara ya kukagua taasisi zilizo chini ya wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na kubadilishana uzoefu na viongozi wa wizara hiyo (Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji) kwa upande wa Zanzibar.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com