RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed
Shein, ametoa taarifa rasmi ya Serikali kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa
Zanzibar wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi.
Katika
taarifa hiyo aliyoitoa jana kupitia vyombo vya habari, Alhaj Dk. Shein
kwa masikitiko makubwa aliwaarifu wananchi kuwa jana tarehe 14 Agosti
2016, Mzee Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia, msiba ambao
umetokea nyumbani kwake Mji Mwema, Dar es Salaam.
Alhaj
Dk. Shein alieleza kuwa Marehemu Mzee Aboud Jumbe ni Rais Mstaafu wa
Zanzibar wa Awamu ya Pili, ambaye vile vile alikuwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Marehemu Mzee Aboud Jumbe
amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na umri wake.
Kwa
taarifa ya Alhaj Dk. Shein, maziko ya marehemu yatafanyika leo tarehe
15 Agosti 2016 saa 7.00 mchana ambapo maiti yake itasaliwa katika Masjid
Mshawar, Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani kwake Migombani.
Aidha,
Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa kufuatia mchango na juhudi kubwa ambazo
Marehemu Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi alizichukua katika uhai wake kwa
kuitumikia, kuiongoza na kuijenga Zanzibar pamoja na nafasi yake katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nchi yetu imekabiliwa na msiba mkubwa kwa kifo cha kiongozi huyu mahiri”alieleza Alhaj Dk. Shein katika taarifa hiyo.
Kutokana
na msiba huo mkubwa Alhaj Dk. Shein alitangaza rasmi siku saba za
maombolezo, kuanzia leo tarehe 15 Agosti 2016 ambapo katika kipindi
hicho chote bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Pamoja
na hayo, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa utaratibu wa maziko utafuata
wasia ambao mwenyewe marehemu aliutoa wakati wa uhai wake.
“Tunaungana
na Wanafamilia wote katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Naomba
kutumia nafasi hii kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wote. Tunamuomba
Mwenyezi Mungu amjaalie kauli thabit marehemu mzee wetu na amlaze pahala
pema peponi, Amin. Inalillahi wainnailaihi rajiun” Alieleza Alhaj Dk. Shein katika Taarifa hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 comments:
Post a Comment