Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), Eng. Steven Mlote
akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu maadhimisho ya
14 ya Siku ya Wahandisi Tanzania itakayoadhimishwa Septemba mosi jijini
Dar es Salaam.(Picha Zote Na Benjamin Sawe – Maelezo).
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya kumi na nne ya Siku
ya Wahandisi yatakayofanyika Septemba mosi hadi pili jijini Dar es
Salaam.
Maadhimisho
hayo ya siku mbili yanatarajiwa kukutanisha zaidi ya wahandisi elfu
mbili kutoka ndani na nje ya nchi ili kupata fursa ya kufanya
majadiliano ya kitaaluma, kufanya maonesho ya kiufundi na kibiashara,
kuwatambua na kuwazawadia wahandisi wahitimu waliofanya vizuri katika
mafunzo yao ya mwisho na kuwaapisha wahandisi waliokidhi vigezo.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam, Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), Eng.
Steven Mlote amesema mada kuu katika maadhimisho hayo itakuwa ni
“TANZANIA KUELEKEA KUWA NCHI YA UCHUMI WA KATI NA KUWA NCHI YA VIWANDA:
NINI JUKUMU LA WAHANDISI”.
“Tumejipanga
Siku ya Wahandisi mwaka huu iwe na mvuto wa pekee kwa sababu mada yake
ni ya kitaifa ikiangalia Dira ya Maendeleo ya Taifa na mwelekeo wa nchi
kuwa nchi ya viwanda” amesema Eng. Mlote.
Maadhimisho
ya wahandisi Tanzania yamekuwa yakifanyika tangu mwaka 2013, lengo
likiwa ni kuiwezesha jumuiya ya wahandisi nchini kuionesha jamii kile
ambacho wahandisi wanaweza kukifanya katika kuleta maendeleo ya nchi.
Takribani
wahandisi elfu 17 wanakadiriwa kuwepo nchini katika sekta mbalimbali,
lengo likiwa ni kuwa na wahandisi elfu 83 ili kukidhi mahitaji ya nchi
kuwa ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
0 comments:
Post a Comment