METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, August 18, 2016

Rais Magufuli Akutana Na Katibu Mkuu Msaidizi Wa Umoja Wa Mataifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 18 Agosti, 2016 amekutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Balozi Liberat Mfumukeko Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumsihi ahakikishe Jumuiya inajielekeza kukabiliana na matatizo ya wananchi na kupunguza matumizi ya fedha yasiyo ya lazima.

Dkt. Magufuli amesema ni vema Jumuiya hiyo itilie mkazo katika kuziwezesha nchi wanachama kukabiliana na matatizo muhimu ya wananchi yakiwemo upatikanaji wa maji, uboreshaji wa miundombinu kama vile barabara na reli, kuimarisha huduma za afya, kujenga viwanda vitakavyozalishaji ajira na kuongeza mapato, na kukuza biashara na uwekezaji.
"Itakuwa ni manufaa zaidi endapo nyie watendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mtafanya juhudi kubwa kuhakikisha nchi wanachama zinajikita kukabiliana na matatizo ya wananchi, mkifanya hivyo na mkaepuka matumizi makubwa ya fedha kwenye mambo yasiyo ya lazima tutanufaika zaidi" Amesema Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amempongeza Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, aliyeshika wadhifa huo kuanzia Mwezi Aprili mwaka huu (2016) kwa mipango na mikakati mizuri aliyoanza nayo katika kutekeleza malengo ya Jumuiya ikiwemo kupunguza matumizi, kuvutia wawekezaji na kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi na programu iliyo chini ya Jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Liberat Mfumukeko pamoja kumshukuru Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwake ameahidi kutekeleza wajibu wake vizuri na kwa manufaa ya wana Afrika Mashariki.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya idadi ya watu hapa nchini (UNFPA - Tanzania) Dkt. Natalia Kanen ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UNFPA.

Dkt. Magufuli amempongeza Dkt. Natalia Kanen kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na amesema anaamini kuwa Dkt. Natalia Kanen atakuwa Balozi mzuri wa Tanzania hususani katika kuongeza mkazo kwa Umoja wa Mataifa kuisadia Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali  zikiwemo ongezeko la wakimbizi, umasikini na huduma za mama na mtoto.

Kwa upande wake Dkt. Natalia Kanen ambaye amekuwa hapa nchini kwa kipindi cha takribani miaka miwili ameishukuru na kuipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya amani na jinsi ilivyojitoa kuwahudumia wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali yanayokumbwa na matatizo ikiwemo mapigano.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
18 Agosti, 2016
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo wakati akizungumza na Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya Watu UNEPA, Dkt. Natalia Kanem na ujumbe wake
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akitazama vitabu alivyopewa na mgeni wake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya Watu UNEPA, Dkt. Natalia Kanem mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.wengine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Katibu Mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Liberat Mfumukeko Ikulu jijini Dar es salaam Agosti 18,2016.PICHA NA IKULU
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com