Ndege za
kijeshi za Marekani zimezishambulia ngome za wanamgambo wenye itikadi
kali wa kundi la Dola Kiislamu IS katika mji wa Sirte nchini Libya
kufuatia ombi la serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Mashambulizi
hayo ya angani yaliyofanywa hapo jana yametajwa na maafisa wa Marekani
kuwa mwanzo wa kampeni kabambe dhidi ya wanamgambo hao wa IS mjini
Sirte.
Akihutubia
kupitia kituo cha televisheni cha serikali, Waziri mkuu wa Libya Fayez
Serraj amesema mashambulizi ya kwanza yalilenga maeneo maalum
yanayodhibitiwa na IS na kusababisha hasara kubwa kwa majihadi hao.
IS inaudhibiti Sirte tangu mwaka jana
Tangu
mwezi Mei, majeshi tiifu kwa serikali ya muungano ya Libya yamekuwa
yakipambana dhidi ya IS mjini Sirte, mji alikozaliwa aliyekuwa kiongozi
wa Libya Muammar Gaddafi.
Wanamgambo
hao waliiudhibiti mji huo wa pwani mwaka jana na kuifanya ngome yao
kubwa zaidi nje ya Syria na Iraq, lakini sasa wanazingirwa katika maeneo
muhimu mjini humo.
Waziri
Mkuu Serraj amesema wameamua kushiriki katika muungano wa kimataifa
unaopambana dhidi ya IS na kuiomba Marekani kuisaidia kwa kufanya
mashambulizi ya angani dhidi ya maeneo maalum yanayodhibitiwa na IS.
Msemaji
wa wizara ya ulinzi ya Marekani Peter Cook amesema mashambulizi hayo ya
Jumatatu yaliyoidhinishwa na Rais wa Marekani Barack Obama yaliharibu
kifaru na magari mawili ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu.
Cook
amesema katika siku za usoni kila shambulizi litakuwa ni kwa ushirikiano
na serikali ya muungano wa kitaifa ya Libya na itahitaji idhini ya
kamanda wa jeshi la Marekani anayesimamia vikosi vilivyoko Afrika.
Hili ni
shambulizi la tatu la angani lililofanywa na Marekani dhidi ya
wanamgambo walioko Libya lakini maafisa wa Marekani wamesema shambulizi
la jana linaashiria mwanzo wa kampeni kali ya mashambulizi ya angani.
Marekani yanuia kurejesha usalama Libya
Ikulu ya
rais wa Marekani imesema msaada kwa Libya utakuwa tu ni mashambulizi ya
angani na kutoa taarifa za kijasusi kama sehemu ya mipango ya kurejesha
uthabiti na usalama Libya.
Kukombolewa
kwa mji wa Sirte ulioko kilomita 450 mashariki ya mji mkuu Tripoli,
kutakuwa ni pigo kubwa kwa IS ambao wanakabiliwa pia na changamoto kubwa
za kuendelea kuyadhibiti maeneo makubwa Syria na Iraq. Juhudi za
kuukomboa mji huo zimesababisha vifo vya takriban wanajeshi 280 wa Libya
na kuwajeruhi zaidi ya 1,500.
Kulingana
na ripoti iliyowasilishwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki
Moon kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, kuna kati
ya wapiganaji 2,000 na 5,000 wa IS katika miji ya Sirte, Tripoli na
Derna wanaotokea Libya, Tunisia, Algeria, Misri, Mali, Morocco na
Mauritania.
0 comments:
Post a Comment