METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, August 18, 2016

DC MTATURU AMALIZA MGOGORO ULIOCHELEWESHA MRADI WA UMEME WA KILOVOLTI 400

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwa kwenye picha ya pamoja na wananchi wa Kijiji cha Nkui, sawia na baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya ya ikungi mara baada ya kumalizika kwa mgogoro
 Dc Mtaturu akisisitiza jambo wakati wa kikao cha maridhiano
 Dc Mtaturu akielezea faida ya mradi wa umeme wa Kilovolti 400 njia ya Iringa- Shinyanga
 Dc Mtaturu  akizungumza na wananchi waliofika kumlaki baada ya kusikia amezuru kijijini hapo
Umakini unahitajika kutekeleza dhana ya Hapa Kazi Tu

Na Mathias Canal, Singida

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amemaliza mgogoro baina ya serikali ya kijiji cha Nkui kilichopo Kata ya Issuna pamoja na mwananchi Jonas Martin Bahali uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa dhidi ya Tanesco katika mradi wao wa umeme wa Kilovolti 400 njia ya Iringa- Shinyanga.

Kikao hicho cha pamoja kwa ajili ya maridhiano kimeimarisha uelewano kati ya kijiji na mwananchi huyo ambaye kwa kiasi kikubwa hakupatiwa elimu nzuri juu ya umuhimu wa mradi huo kwa Wilaya ya Ikungi, Mkoa,Taifa na kwa mwananchi mmoja mmoja kuelekea Tanzania ya viwanda kwani ndio umeme wenye uwezo mkubwa kuhimili viwanda vikubwa nchini.

Awali serikali ya kijiji na mwananchi huyo baada ya kusuluhishwa waliamua kugawana eneo husika nusu kwa nusu ambapo hata hivyo Serikali ya kijiji pamoja na mwananchi huyo walizuia kuendelea kwa mradi mpaka pale watakapolipwa fidia ya eneo lao lenye thamani ya shilingi milioni kumi na laki sita (10,600,000) ambapo kila mmoja atalipwa shilingi milioni tano na laki tatu 5,300,000).


Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya Dc Mtaturu  aliwafafanulia wajumbe wa Serikali ya kijiji na ndugu Bahali kuwa mpaka sasa hawajalipwa fidia kutokana na kukosewa kwa majina yao katika malipo ya awali.

Amesema kuwa malipo ya awali yalionesha kuwa Ndugu Yona S. Njiku na ndugu Jonas Njiku ndio waliotakiwa kulipwa lakini ukweli ni kwamba watu hao hawapo katika Kijiji cha Nkui jambo ambalo limeleta sintofahamu na kusitishwa kwa malipo.

Kupitia kukosea kwa majina hayo kulipelekea Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Singida aliyekuwa anasimamia jambo hilo kuamua kurudisha kiasi cha shilingi milioni kumi na laki sita (10,600,000) kwenye Shirika la Umeme TANESCO baada ya kukosa watu wa kuwalipa.

Baada ya mazungumzo hayo yaliyozaa maridhiano Mkuu wa Wilaya aliwaomba wajumbe pamoja na Bwana Bahali kuruhusu mradi huo kuendelea na kuahidi kuhakikisha anasimamia ili wananchi husika waweze kulipwa stahiki zao.

Hata hivyo kisa cha wananchi hao kuzuia mradi huo wameeleza wasiwasi wa fedha hizo kubwinywa na badhi ya viongozi Kijijini hapo kama ilivyofanywa kwa fedha zilizolipwa hapo awali ambapo wajumbe walitolea mfano wa shilingi milioni tisa zinazodaiwa kutumiwa vibaya na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mayuta iliyopo Kijiji cha Nkui, Wilayani Ikungi.

Msimaizi wa mradi wa umeme wa Kilovolti 400 unaotoka Iringa kuelekea Shinyanga Lawrance M. Njuani aliahidi mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi kuwa malipo ya fidia ya wahusika yatakuwa tayari ndani ya mwezi mmoja.

Sambamba na hayo pia Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi aliwakumbusha wajumbe wa serikali ya Kijiji kuhusu wajibu wao wa kusimamia shule na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili huku akiahidi kulitafutia majawabu suala zima la tuhuma za Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mayuta.

Huu ni mgogoro wa pili kumalizwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu tangu awasili Wilayani hapo baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Msaidizi wake katika Wilaya hiyo ambapo hivi karibuni alimaliza Mgogoro uliodumu katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi kati ya wananchi wa Kijiji cha Mang'oni na Muwekezaji Shanta Gold Mine.


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com