Neno La Wakati Mwema
Na Mathias Canal
Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu ndugu zangu katika Lymaan...! Naamini afya zetu zinazidi kuimarika lakini kwa wale ambao kwa namna moja ama nyingine afya zao zimedhoofu nawapa pole na kuwatakia Buheri ili muweze kuimarika na kuendelea majukumu ya jamii na Taifa ili yazidi kukolea.
Leo nimewiwa kumzungumzia mwanamke mwenye heshima kubwa ya Jinsia yake lakini pia Wanawake ni mama zetu, dada zetu, wake zetu, wadogo zetu, shemeji zetu, shangazi zetu lakini pia ni Nyanya (bibi) zetu.
Kwa mujibu wa mtandao wa http://daily-helper.com/sw/276015 imeelezwa vyema historia ya kimataifa ya wanawake ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Machi 8, Imeelezwa vyema sana na mtandao huu kuwa maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kwa mara ya kwanza yalifanyika Februari 28, 1909 huko Marekani
Umoja wa Mataifa wenyewe umesema siku hii ni ya kutafakari juu ya hatua za kimaendeleo ambazo wanawake wamepiga, kupongeza juhudiza wanawake wa kawaida kutokana na mchango wao katika historia ya maendeleo ya nchi na jamii zao
Kauli mbiu ya mwaka huu kuadhimisha siku hii ya wanawake ni
“Usawa kwa wanawake ni
maendeleo kwa wote.”
Kauli mbiu hii inasisitiza usawa wa kijinsia kuwawezesha wanawake kupata haki zao za kibinadamu, kutokomeza umasikini na kuwainua katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Lakini pia upo mtazamo wa 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030.
Binafsi nawaheshimu na kutambua umuhimu wa wanawake kwa sababu shuruba wazipatazo kuwalea watoto wetu ndizo shuruba alizozipata mama yangu kunilea mimi.
Mwanamke si mtu wa kubezwa kama ilivyo desturi na mtazamo wa wengi kwamba mwanamke hawezi kufanya jambo lolote kama hatawezeshwa...Hii ni dhana mfu tena iliyopitwa na wakati tumejionea wanawake wangapi ambao wanawawezesha wanaume tena bila hata wao kuwezeshwa.
Kuishi kwa kukariri ni hatari kwa ustawi wa maisha yetu hivyo ni vyema kama tutaishi kwa kujifunza maana hata tafsiri ya maisha nyepesi ni ile ya maisha ni kuishi na kujifunza.
Katika Jamii zetu mara kadha yameripotiwa matukio mbalimbali ikiwemo yale ya kuwanyanyapaa wanawake, kuwapiga lakini yapo pia matukio ovu kabisa ya kuwabaka wanawake.
Mwanamziki nguli kabisa nchini Tanzania Suleimani Msindi (Afande Sele) aliwahi kusikika katika moja ya mashairi yake akisema Mwanamke kama hataki usimbake mwache aende zake mana kulazimisha penzi ni hatari sawa na kulazimisha fani kisha unaleta utani.
Afande Sele aliimba kwa kumaanisha lakini wanaume wengi wamekuwa wakilazimisha penzi kwa wanawake pasina maandalizi yoyote yale badala yake kusukuma hisia za kimwili kilazima. Hii ni dhambi kubwa mbinguni na duniani pia ikemewe tena ishindwe na kulegea milele.
Lakini Nitamatishe Neno La Wakati Mwema kwa kuwakumbusha wanawake kwa uchache yale muhimu wapaswayo kufanya ikiwa ni pamoja na kuvumilia kutunza mimba miezi tisa kuliko kutoa na kukiua kiumbe muhimu kisicho na hatia, Lakini pia watambue kuwa mtoto wa mwenzio ni wa kwako tusiwatenge, Lakini kwa wale wanawake (Mashangingi) ambao kazi yao ni kutafuta pesa na kurubuni vijana wadogo kufanya ngono kama ujira kisa mshiko na hatimaye kuwafanya vijana hao kuwa Mariot waache tabia hizi kwa ustawi wa Taifa na heshima kwa wanawake wengine na vijana kama mimi.
Naam, Wanawake ni jeshi kubwa hilo nalitambua, wanawake wanahitaji Love (Mapenzi), Care (Kuwajali) na Respect ( kuwaheshimu). Lakini zawadi pekee kutoka kwa wanaume kwenda kwa watoto ni kumpenda mama yao.
Ni Neno La Wakati Mwema
Mathias Canal Mnyiramba
0756413465
Mabibo-Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment