Licha
ya Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) kueleza kusikitishwa kwao na
uchaguzi wa marudio Zanzibar kufanyika bila kuwapo maelewano ya pande
zinazokinzana, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia kushiriki,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema iko tayari kufa njaa
kuliko kukubali kuingiliwa uhuru wake.
Juzi,
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
alimtangaza Dk. Ali Mohamed Shein, mshindi wa uchaguzi wa marudio
uliofanyuika Jumapili iliyopita, kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4,
hatua iliyozifanya balozi mbalimbali nchini kueleza maskitiko yao na
kusisitiza kuwa ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na
unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu.
Tamko
la mabalozi hao lilitolewa na wawakilishi wa nchi za Ubelgiji, Canada,
Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia,
Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Switzerland, Uingereza na Marekani.
Wakati
kauli ya mabalozi hao ikizua hofu kuwa huenda Zanzibar na Tanzania kwa
ujumla ikakatiwa misaada na mikopo kutoka nje, kwa madai ya kupindishwa
kwa demokrasia, SMZ imetoa msimamo kwamba haitazipigia magoti nchi
wahisani na kwamba imeanza kujipanga kujitegemea kwa mapato ya ndani
katika bajeti yake.
Msimamo
huo wa SMZ, ulitolewa jana kwa nyakati tofauti na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, na Waziri wa
Fedha wa Zanzibar, Omary Yusuph Mzee, walipozungumza kuhusu msimamo wa
EU, Marekani na washirika wao kusikitishwa na kurudiwa uchaguzi kabla
ya kupatikana muafaka wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.
Aboud
alisema uchaguzi wa marudio umefanyika Zanzibar ikiwa utekelezaji wa
masharti ya katiba na sheria na haikuwa muafaka kwa wahisani kuhoji
kufanyika kwake.
“Kitendo
wanachokifanya washirika wetu wa maendeleo hakikubaliki katika misingi
ya utawala wa sheria. Wanaingilia mambo ya ndani wakati Zanzibar ni nchi
huru,”alisema Aboud.
Alisema
uchaguzi wa Zanzibar unaendeshwa kwa kufuata masharti ya katiba na
sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984 na si maridhiano ya vyama,
kama wanavyotaka wahisani.
Aboud
alisema Zanzibar iko tayari kushirikiana na washirika wa maendeleo,
lakini lazima misaada izingatie utu na heshima ya nchi kwa manufaa ya
Zanzibar na wananchi wake.
“Zanzibar
ni nchi huru na itaendelea kuwa huru. Tuko tayari kupokea misaada
inayozingatia utu na heshima kwa Zanzibar na wananchi wake kinyume cha
hivyo tuko tayari kufa njaa,” alisisitiza.
Naye
Mzee kwa upande wake, alisema jana ofisini kwake, Vuga, visiwani hapa
kuwa hategemei hilo kutokea katika kipindi cha miaka mitano kuanzia
sasa.
Alisema
lengo la serikali kwa sasa ni kuhakikisha inaondokana na utegemezi wa
wafadhili na kwamba imeanza kuweka mikakati maalum, kuhakikisha
inajitosheleza kwenye bajeti yake.
Alisema
miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kufanywa kutimiza lengo hilo ni
kuanza kuiga mfumo anaoutumia Rais John Magufuli wa kufuta safari
zisizokuwa za lazima kwa viongozi wa serikali.
Aliongeza
kuwa mikakati mingine ni kuhakikisha wagonjwa wanaotakiwa kwenda
kutibiwa nje ya nchi, wanapata huduma hiyo nchini kwa kuandaa mipango
maalum ya kuleta madaktari.
Mzee
ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, alisema Zanzibar inatarajia kutumia mapato yake ya ndani
kujitosheleza kwenye bajeti yake.
Alisema
Rais Dk. Shein juzi alitoa msimamo wa serikali wa kutaka iwekwe
mikakati itakayowezesha Zanzibar kujiendesha kwa bajeti yake bila
wafadhili.
Mzee
alisema Zanzibar inategemea asilimia 20 ya misaada kwa ajili ya
kukamilisha bajeti yake kila mwaka pamoja na mikopo kutoka taasisi za
fedha, zikiwamo benki za nje.
Alisema
bajeti ya Zanzibar inategemea asilimia 26 hadi28 ya mapato yanayotokana
na sekta ya utalii wa ndani na nje na kwamba bado kunahitajika mikakati
ili kupanua wigo wa kupata fedha.
Kwa
mujibu wa Mzee, Zanzibar inapokea watalii kati ya 300,000 na 400,000
kwa mwaka na kwamba wanatarajia kuongezeka baada ya kufungua ofisi za
kuhamasisha utalii wa nje.
Alisema
ofisi maalum za kuhamasisha utalii zimejengwa katika mji wa Mumbai,
India na nchini China na kwamba kwa sasa watalii wanatoka moja kwa moja
kwao na kufikia Zanzibar.
Kwa
upande wa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, Mzee alisema unatarajia kukua
kwa asilimia 8 hadi 10 kwa mwaka na kwamba tofauti za kisiasa zilizopo
Zanzibar haziwezi kuathiri mipango ya serikali.
Katika
hatua nyingine, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ali Ameir
Mohamed, alisema haikuwa muafaka EU na Marekani kusikitishwa na
kufanyika kwa uchaguzi wa marudio.
Alisema
ZEC ilikuwa na kila sababu za kuitisha uchaguzi wa marudio ili
kukamilisha masharti ya katiba, baada ya uchaguzi wa awali kuvurugika.
Mwanasiasa
huyo alisema matatizo ya kisiasa ya Zanzibar yaliachwa na wakoloni
wenyewe kutokana na matabaka waliyokuwa wameyajenga kabla ya kufanyika
kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Alisema
wahisani jukumu lao kubwa ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika
nchi wanazoziwakilisha na si kuingilia mambo ya ndani.
Credit: Nipashe
0 comments:
Post a Comment