Jaji Mstaafu Joseph Warioba amesema uamuzi wa serikali ya awamu ya
tano wa kuanzisha mahakama itakayoshughulikia ufisadi, rushwa na uhujumu
uchumi umekuja wakati muafaka lakini amependekeza kuwa mahakama pekee
haiwezi kushughulikia suala hilo bila kushirikiana na Jeshi la Polisi na
Takukuru. Jaji Warioba amesema hayo leo wakati alipoalikwa Wizara
ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kutoa maoni na mapendekezo yake
kuhusiana na serikali kuanzisha mahakama itakayoshughulikia Rushwa na
wahujumu uchumi.
“Mahakama pekee haiwezi kushughulikia ufisadi na
uhujumu uchumi bila kushirikisha vyombo vingine ambavyo ni Jeshi la
Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika kuimarisha
mahakama hiyo ambayo inatarajia kuanzishwa hivi karibuni” amesema Jaji
Warioba.
Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha utaratibu wa
kukutana na viongozi wa zamani ambao walishawahi kuongoza wizara hiyo
kwa lengo la kupata mapendekezo, maoni na uzoefu juu ya kuanzishwa kwa
mahakama.
“Leo nimekaribishwa wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo
la kubadilishana mawazo kuhusiana na uanzishwaji wa mahakama
itakayoshughulikia ufisadi, rushwa na wale wanao hujumu uchumi, huu ni
uamuzi mzuri na hizi ni jitihada za wazi za serikali katika kupambana na
rushwa”amesema Jaji Warioba.
Amesema lengo la serikali la
kuanzisha kwa mahakama hiyo ni kupambana na ufisadi na tayari serikali
ya awamu ya tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kuzuia mianya ya rushwa
katika ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake, Waziri wa Sheria na
Katiba , Dk Harrison Mwakyembe amesema katika kipindi kifupi cha uongozi
wa rais Magufuli masuala yote ya msingi aliyoyasema wakati wa kampeni
ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana ameshaanza kuyatekeleza.
“Uanzishwaji
wa mahakama itakayoshughulikia ufisadi na uhujumu uchumi ni miongoni
mwa vipaumbele alivyovitoa rais Magufuli wakati wa kampeni hivyo kwa
kiasi kikubwa yale yote ambayo aliahidi kipindi cha uchaguzi ameanza
kuyatekeleza”amesema Dk Mwakyembe.
Amesema mbali na uanzishwaji wa
mahakama hiyo, pia suala la katiba mpya litashughulikiwa lakini kwa
kuanza rais Magufuli ameanza na kuwawajibisha wale wote ambao wamekiuka
maadili ya kazi zao pamoja na kuanzisha mahakama itakayoshughulikia
ufisadi na uhujumu uchumi.
0 comments:
Post a Comment