Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais wa
Vietinam, Trung Tan Sang kuhutubia mkutano wa biashara na uwekezaji kati
ya Tanzania na Vietinam kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Julius Nyerere jijini Dar es salaam Machi 9, 2016. (Picha na ofisi ya
Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mabadiliko ya kiuchumi yaliyofanyika nchini
yameifanya Tanzania ipige hatua kubwa katika kipindi cha miaka 10
iliyopita.
“Kumekuwa
na mabadiliko chanya kwenye ukuaji halisi wa Pato la Taifa, kushuka kwa
mfumuko wa bei, na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni. Pato la Taifa
limekua kwa wastani wa asilimia 7 na mfumuko wa bei umeshuka hadi
kufikia asilimia 5.3 mnamo Juni 2015 ikilinganishwa na asilimia 16 na
asilimia 8 ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka 2012 na mwanzoni wa mwaka
2013,” alisema.
Ametoa
kauli hiyo leo jioni (Jumatano, Machi 9, 2016) wakati akihutubia
kongamano la biashara baina ya Tanzania na Vietnam lililofanyika kwenye
ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Bw. Troung
Tan Sang.
Akizungumza
kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema mbali
ya mabadiliko ya kiuchumi, Tanzania pia imefanya mabadiliko kwenye
sheria, mifumo ya kifedha na sekta za kuhudumia jamii za umma.
“Katika
kipindi cha muongo mmoja uliopita tumefanya mabadiliko ya kisera na
kwenye sheria zetu ili kuboresha hali ya uwekezaji, kukuza uchumi na
kuboresha maisha ya wananchi,” alisema.
Alitoa
mwaliko kwa wafanyabiashara walioambatana na Rais wa nchi hiyo kwa
kuwaeleza kwamba faida kubwa ya kuwekeza nchini Tanzania ni uwepo wa
soko la uhakika kwa wakazi zaidi ya milioni 300 waishio Mashariki na
Kusini mwa bara la Afrika.
“Tanzania
ni mwanachama wa Jumuiya za Kikanda katika SADC na EAC. Uwepo wake
katika taasisi hizi ni fursa tosha. Pia Tanzania ni lango kwa nchi sita
ambazo hazipakani na bahari. Inasaidia kufanyika biashara katika nchi za
Congo (DRC), Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Uganda,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo, Waziri Mkuu
aliwakaribisha wafanyabiashara hao wawekeze kwenye kilimo cha biashara
na viwanda vya usindikaji ili waweze kusaidia kuongeza uzalishaji wa
chakula nchini.
0 comments:
Post a Comment