Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe
16 Machi, 2016 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha
umeme wa Kinyerezi namba mbili, uliopo katika wilaya ya Ilala Mkoani Dar
es salaam, ambao utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha
megawatts 240 za umeme.
Mradi
huo ambao utazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia inayosafirishwa kwa
bomba kutoka Mtwara, unatarajiwa kuanza kuzalisha umeme katika kipindi
cha kuanzia miezi 21 hadi 28 utakapokamilika kabisa.
Kuanza
kwa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme huo, kunafuatia juhudi
zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano ya kufanikisha upatikanaji wa
shilingi bilioni 120, ikiwa ni asilimia 15 ya fedha zilizopaswa kutolewa
na Tanzania na fedha nyingine shilingi Bilioni 292 zimetolewa na Japan.
Mradi
huu umetanguliwa na mradi wa Kinyerezi namba moja ambao una uwezo wa
kuzalisha megawatts 150 za umeme, na mitambo yake tayari imeanza
uzalishaji wa megawatts 105 zilizoingizwa katika gridi ya Taifa.
Pamoja
na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Kinyerezi namba mbili,
Rais Magufuli amekagua mitambo ya kuzalisha umeme ya mradi wa Kinyerezi
namba moja, ambapo Mkuu wa Kituo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
cha Kinyerezi Mhandisi John Mageni, ametoa maelezo kuwa shirika hilo
lina mpango wa kupanua uzalishaji wa umeme katika mradi huo kutoka
megawatts 150 hadi kufikia megawatta 335, kwa kuongeza mitambo ya kufua
umeme kwa teknolojia inayojumuisha matumizi ya gesi asilia na mvuke
uzalishwao na mitambo hiyo.
Baadaya
ya kupokea maelezo hayo, Rais Magufuli ameridhia kuwa serikali yake
itatoa Dola za kimarekani milioni 20, kwa ajili ya kufanikisha upanuzi
wa mradi huo na ameagiza kuwa wataalamu wa TANESCO washirikiane na
Mkandalasi kuhakikisha upanuzi huo unafanyika haraka iwezekanavyo,
badala ya muda wa miezi 12 uliopangwa.
Akizungumza
na wananchi waliojitokeza katika sherehe za uzinduzi wa mradi huo, Rais
Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na
TANESCO, kuanza kuachana na mitambo ya kukodi kwa ajili ya kuzalisha
umeme, na badala yake nchi ijenge mitambo yake yenyewe ili kuondokana na
gharama kubwa za nishati hiyo muhimu.
“Waziri,
ukiona mtaalamu anakuletea mapendekezo ya kutaka kukodi mitambo ya
kuzalisha umeme, badala ya kuleta mapendekezo ya kununua mitambo yetu
wenyewe ujue mtaalamu huyo hafai, mtoe” Amesisitiza Rais Magufuli
Ameongeza
kuwa tafiti zimethibitisha kuwa hadi sasa Tanzania ina zaidi ya futi za
ujazo Trilioni 57 za gesi asilia, ambayo itazalisha umeme wa
kutosheleza mahitaji ya ndani, na umeme mwingine kuuzwa nje ya nchi
ikiwemo Kenya ambayo tayari imeomba kuuziwa umeme kutoka Tanzania.
Aidha,
Rais Magufuli ametoa onyo kwa TANESCO kuwa hatarajii kusikia bwawa la
maji la Mtera limeishiwa maji, kwa kuwa katika msimu huu wa mvua maeneo
ya Iringa yalikuwa na mvua nyingi ambazo zimesababisha hadi mafuriko
mafurukio.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema
tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, juhudi zilizofanyika
zimefanikisha kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawatts 800 hadi
kufikia megawatts 1,000 kiasi ambacho ni pungufu kwa megawatts 20 tu,
ikilinganishwa na mahitaji ya megawatts 1020 za sasa.
Ameongeza
kuwa pamoja na kuweka jiwe la msingi la mradi wa Kinyerezi namba mbili,
hivi karibuni serikali inatarajia kujenga miradi mingine ya kuzalisha
umeme kwa kutumia gesi asilia, ikiwemo Kinyerezi namba tatu
utakaozalisha megawatts 600, Kinyerezi namba nne utakaozalisha megawatts
300, na mingine itakayojengwa Lindi na Mtwara.
Prof.
Muhongo amebainisha kuwa mpaka sasa gesi asilia inazalisha kati ya
asilimia 50 na 60 ya umeme wote hapa nchini, Maji yanazalisha asilimia
30 hadi 40, na umeme unaozalishwa kwa mafuta hauvuki asilimia 10.
Sherehe
hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa Japani
hapa nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida, Wabunge wa kamati ya Nishati na
Madini, wafadhili wakiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Afrika na Shirika
misaada la Japan (JICA.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
16 Machi, 2016
0 comments:
Post a Comment