METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 8, 2016

Waliosimamishwa Kazi NIDA Waandamana Kudai Haki Zao

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wameandamana kupinga kitendo cha mamlaka hiyo kuvunja mikataba yao huku wakidai mishahara ya miezi mitatu.
 Wafanyakazi hao walichukua hatua hiyo jana, siku moja baada ya Kaimu Mkurugenzi wa Nida, Dk Modestus Kipilimba kutangaza kuvunja mikataba ya wafanyakazi 597 kwa sababu ya ufinyu wa bajeti na kuongeza ufanisi katika mamlaka hiyo. 
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Dk Kipilimba alikiri wafanyakazi kudai mishahara yao ya miezi mitatu na kuwa ameshapeleka maombi ya fedha serikalini na muda wowote watawalipwa stahiki zao. 
Wafanyakazi hao walisema mkurugenzi huyo amefanya uamuzi huo kwa kukurupuka bila kukaa nao na kuzungumza jinsi gani watalipwa stahiki zao kabla ya kuvunjwa kwa mkataba huo. 
Mtaalamu wa takwimu, Joseph Mtitu alisema alishangazwa na taarifa za kuvunjiwa mkataba wake wakati anadai mishahara ya miezi mitatu. 
Kijana huyo ambaye alikuwa anafanya kazi ya kuingiza taarifa za wananchi kwenye mfumo wa data, alisema mkurugenzi amefanya kazi na vyombo vya habari badala ya kukaa na wafanyakazi wake. 
“Hajafuata taratibu, alitakiwa kutupa taarifa na kuhakikisha kwamba anamaliza madeni yote ndipo avunje mikataba... hatumuelewi,” alisema Mtitu. 
Kijana huyo alisema waathirika wengi kati ya waliovunjiwa mikataba ni vijana ambao wengine wana familia zao akisema kitendo hicho kinaweza kusababisha baadhi yao kujiingiza kwenye vitendo vya ujambazi na ukahaba ili kuendesha maisha yao. 
Mfanyakazi mwingine, Bhoke Mafube alisema Nida imekuwa ikiwakata fedha za mifuko ya jamii ambako walijiandikisha, lakini wakienda kuuliza huko wamekuwa wakiambiwa wao si wanachama na fedha zao hazipo.
 Akizungumzia sababu ya ufanisi mdogo, Peter Michael alisema tatizo hilo siyo lao, bali ni ufinyu wa rasilimali uliosababishwa na uongozi wenyewe. 
Hata hivyo, alisema hiyo si sababu ya kukiuka taratibu na haki za wafanyakazi kwa kuvunja mikataba yao kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu. 
“Tumekuja hapa viongozi hawataki kuzungumza, sijui tutafikiaje muafaka kama wanafanya hivi. 
Sisi siyo watoto wadogo, madai yetu ni ya msingi. Watulipe mishahara yetu ndiyo tuanze kujadili uhalali wa kuvunja mkataba,” alisema mfanyakazi huyo wa Nida. 
Akifafanua madai hayo, Dk Kipilimba alisema mamlaka yake haina fedha kwa sasa ndiyo maana ameamua kuvunja mikataba ya wafanyakazi hao. Alisema njia pekee ilikuwa ni kuvunja mikataba hiyo ili deni lisiendelee kuongezeka.
 Alisisitiza kwamba haki ya mtu haipotei na kuwa atasimamia kikamilifu suala hilo ili kila mfanyakazi apate haki yake.
 “Ni kweli kwamba wafanyakazi hao hawakulipwa mishahara yao ya miezi mitatu kwa sababu hakuna fedha. Nitahakikisha wanalipwa fedha hizo lakini kwa sasa hakuna kazi. 
Hebu fikiria, tuna kompyuta 150 tu wakati wafanyakazi hao wako 597, hatuwezi kwenda,” alisema Dk Kipilimba. 
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa lengo la mamlaka yake ni kutengeneza vitambulisho vya kila mwananchi na siyo kutoa ajira kwa watu hata kama hakuna kazi za kufanya.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com