Rungu la kuwatumbua majipu watumishi wa umma wasiowajibika limetua kwa Mhandisi wa Maji Wilaya ya Chato, Peter Ngolemi baada ya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa kuagiza kusimamishwa na kuamuru Takukuru kumchunguza kutokana na kumdanganya. Ngolemi, anadaiwa kumdanganya Majaliwa kuhusu mradi wa maji katika Kijiji cha Kalebezo ambao umesababisha wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
Mradi huo umesimama tangu mwaka 2011, kutokana na kukosa usimamizi baada ya mashine mbili kutofanya kazi. Licha ya kumsimamisha, Waziri Mkuu aliagiza Takukuru kumchunguza na kumchukulia hatua za kisheria.
“Hatuwezi kuwa na kiongozi muongo, naondoka naye. Mtumishi huyu atakaa pembeni Takukuru wamchunguze,” alisema.
Kabla ya kuchukua uamuzi huo, Majaliwa alimwita jukwaani na kumtaka ajibu madai ya wananchi kukosa maji muda mrefu.
“Hatuwezi kuwa na kiongozi muongo, naondoka naye. Mtumishi huyu atakaa pembeni Takukuru wamchunguze,” alisema.
Kabla ya kuchukua uamuzi huo, Majaliwa alimwita jukwaani na kumtaka ajibu madai ya wananchi kukosa maji muda mrefu.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna
mashine mbili na hili suala lipo kwa Mamlaka ya Maji Bukoba, lakini zile
pampu mbili zipo,” alijibu Ngolemi huku akitetemeka na wananchi
wakimzomea.
Hatua hiyo ilisababisha Majaliwa kusema: “Huwezi
kumdanganya Waziri Mkuu anayetegemewa na wananchi wengi, nimepita pale
wananchi wana mabango wanadai mashine ziling’olewa na kupelekwa
Morogoro, halafu leo unaniambia zipo!
“Sasa naondoka na wewe, kaa pembeni kuanzia sasa hakuna kazi, Takukuru mchunguze na kumchukulia hatua.”
Baada ya agizo hilo, maofisa wa usalama walimchukua mhandisi huyo na kuondoka naye kwenye Uwanja wa Chato.
Katika
hatua nyingine, Majaliwa ameagiza kufutwa kwa umiliki wa mashamba
makubwa 11 yakiwamo ya Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge yenye ukubwa wa
ekari 7,700 kwenye vijiji vya Kasharazi na Rwakalemera, Wilaya ya Ngara
mkoani Kagera, kutokana na kutokuwa na hati na kutelekezwa kwa muda
mrefu.
Pia, Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Colnel Ngudungi na kutaka
arejeshwe wilayani hapa kujibu tuhuma za kuhusika na upotevu wa fedha za
mauzo ya mbao kwenye Msitu wa Rumasi.
Ngudungi alihamishwa
kwenda Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga Agosti 2015, kwa kile
kilichoelezwa kuwa anakwenda kwa kazi maalumu.
Majaliwa ambaye
alikuwa njiani kuelekea Geita akitokea Kagera, alitoa maagizo hayo jana
alipozungumza na wakazi wa vijiji vya Kasulo na Rwakalemera, baada ya
kusimamishwa na wananchi wakiwa na mabango wakiomba kurejeshewa ardhi ya
kijiji huku baadhi yao wakidai wanatishiwa kwa bunduki wanaposogelea
mashamba hayo.
Waliendelea kuwa uongozi wa kijiji umekithiri kwa
ubadhirifu kwani licha ya Msitu wa Rumasi kuuzwa na mapato kutoonekana,
kijiji kina minada ya ng’ombe ambayo sheria inataka asilimia 20 ya
mapato ibaki eneo hilo.
Awali, Waziri mkuu alimuita kwenye
mkutano huo Ofisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya, Betty Munuo ili aeleze
chanzo cha mgogoro wa ardhi katika vijiji hivyo.
Akitoa
ufafanuzi huo, Munuo ambaye amehamishiwa wilayani hapo Agosti mwaka
jana, alisema malalamiko hayo ameyarithi kwa mtangulizi wake na amefanya
uchambuzi wa majina ya wamiliki wote wa mashamba na kwamba, uongozi wa
wilaya ulikuwa unapanga kuwapatia notisi ya kujieleza.
Munuo alisema kati ya wamiliki 18 wa mashamba makubwa, saba ndiyo wenye hati huku matatu pekee ndiyo yameendelezwa.
Kwa
mujibu wa Munuo, mashamba yaliyoendelezwa yanatumika kwa kilimo,
ufugaji na shule na kwamba Shamba namba 606 lenye ukubwa wa ekari 161
linamilikiwa na Kanisa Katoliki Dayosisi ya Rulenge, Dario Zakaria
shamba ana ekari 282 na Masista wa Mtakatifu Fransisco wanamiliki ekari
759.
“Mashamba manne ndiyo yenye hati lakini yametelekezwa,
yaliyotelekezwa yote yapo Kijiji cha Rwakalemera nayo ni ya Abdallah
Sadalla (ekari 521); Mahsen Saidi (458); Mshengezi Nyambele (3,88) na
Mushengezi Nyambele (497).
Majaliwa aliwataja wamiliki wa
mashamba yasiyo na hati kuwa ni Joseph Rugumyamheto (505) lipo
Rwakalemera, Nicholaus Kidenke, Gwasa Angas Sababili (236) lipo
Kasharazi na Makumi Rufyega (500) lipo Rwakalemera.
Wamiliki
wengine ambao mashamba yao yapo kijiji cha Rwakalemera na ukubwa wake
kwenye mabano ni Paulo Shikiri (250), Frank Derila (750), Godfrey
Kitanga (800), Phillemon Mpanju (200), Issa Sama (500), Hekizayo
Mtalitinya (225) na Joel Nkinga (1,250).
Majaliwa aliagiza
kurejeshwa mara moja aliyekuwa Ofisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Enock Mponzi
ambaye amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara ili aende
kusaidia uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment