Karatasi za kupigia kura kwa ajili ya marudio ya uchaguzi wa Zanzibar
unaotarajiwa kufanyika Machi 20, ziliwasili jana mchana visiwani hapa.
Karatasi hizo zilipokewa na watendaji mbalimbali wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), wakiongozwa na mkurugenzi wake, Salim Kassim katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Mkurugenzi huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa jumla ya karatasi 5,385 ndizo zilizowasili.
Kassim
alisema karatasi hizo zimechapishwa katika kiwanda cha Unprint cha
Durban, Afrika Kusini na ziliwasili hapo kwa ndege yenye Na EW-364TG ya
nchi hiyo. Alisema karatasi hizo pamoja na vifaa vingine vitasambazwa
vituoni Machi 18, mwaka huu.
Kassim alisema katika karatasi hizo
za kupigia, yapo pia majina ya wagombea wote tisa wa vyama vya upinzani
waliokwishatangaza kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio.
Miongoni mwa wagombea hao ni Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF, ambaye ametangaza kujitoa.
Uchaguzi huo wa marudio, pia unaelezwa kugomewa na waangalizi wa kimataifa na hata wale wa ndani.
Mbali
na CUF vyama ambavyo pia vimeeleza kutoshiriki uchaguzi huo ni Chaumma,
Chama cha Kijaamii (CCK), APPTMaendeleo, ACT-Wazalendo, Jahazi Asilia,
Demokrasia Makini, NRA na SAU.
Kassim alipotakiwa kueleza sababu
za ZEC kuchapisha karatasi za kura zenye wagombea waliotangaza kususia
uchaguzi huo wa marudio, alijibu kuwa yeye si msemaji.
Akizungumzia
gharama za uchaguzi huo wa marudio, mhasibu wa ZEC, Yussuf Ali Hassan
alisema utagharimu Sh4.5 bilioni tofauti na ule wa Oktoba 25, mwaka jana
uliofutwa ambao uligharimu kiasi ya Sh5.3 bilioni.
Picha
za ujio wa Makatarsi na huyo anayeonekana hapo ni Mkurugenzi wa ZEC
Salim Kassim Ali akitoa maelezo ya kuwasili kwake uwanja wa ndege
Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment