Tangu Novemba 5 wakati Dk John Magufuli alipoapishwa, ni Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga pekee
waliotoka nje ya nchi, lakini jana Rais aliwaruhusu mawaziri wengine
wawili kusafiri nje.
Rais Magufuli alizuia safari za nje siku
chache baada ya kuapishwa akisema watumishi wa umma watakaokuwa wakitaka
kwenda nje watalazimika kuomba kibali kutoka Ikulu, ikiwa ni mkakati
wake wa kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali.
Tangu wakati
huo, safari za nje kwa watumishi wa umma zimekuwa za nadra na mawaziri
wamekuwa wakifanya ziara za kwenda mikoani kufuatilia utendaji na utoaji
wa huduma kwa wananchi.
Jana, Rais Magufuli aliwaruhusu
mawaziri wawili kwenda Vietnam kujifunza mbinu za kuinua kilimo na
kujenga viwanda ili kuwaondoa Watanzania kwenye lindi la umaskini.
Mawaziri wawili waliopata kibali hicho ni Waziri wa Viwanda na Biashara,
Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba.
Rais
Magufuli alitoa uamuzi huo jana baada ya kufanya mazungumzo na Rais
Truong Tang Sang wa Vietnam juzi na kukubaliana kuweka sawa mazingira ya
biashara na uwekezaji baina ya nchi zao.
Akizungumza jana baada
ya kumtembeza Rais huyo kwenye Eneo Maalumu la Uwekezaji la Benjamini
Mkapa (EPZ) lililopo Ubungo jijini hapa, Waziri Mwijage alisema Dk
Magufuli ametoa kibali hicho baada ya kuridhishwa na mabadiliko ya muda
mfupi ya Vietnam.
“Kutokana na hatua waliyopiga, Rais
ameniruhusu mimi na Waziri wa Kilimo, Mwigulu Nchemba kwenda nchini humo
muda mfupi baada ya Rais Truong kuondoka.
"Nitakwenda kujifunza mbinu zao ili sekta ya viwanda iajiri zaidi ya asilimia 46 ya vijana wa Kitanzania,” alisema Mwijage.
Baada
ya kuondolewa vikwazo na Marekani, Vietnam ilichagua kuendeleza maeneo
maalumu ya biashara na kufanikiwa kujijenga kiuchumi na kufikia uchumi
wa kati katika kipindi cha miaka 23.
Rais Truong alieleza kuwa waliwekeza Sh10 bilioni katika miradi na asilimia 80 ya fedha hizo ilielekezwa katika mauzo ya nje.
“EPZ
zina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu. Ninaamini, Tanzania inaweza
kupata zaidi ya Dola 20 bilioni kwa mwaka itazipata kutoka katika maeneo
haya.
"Hata sisi wakati tunaanza tulikuwa na EPZ chache lakini
sasa tunazo nyingi na zinatuingizia dola 20 bilioni (za Marekani) kwa
mwaka,”alisema.
Pamoja na eneo hilo, Mwijage alisema Serikali ina mpango wa kuijenga Bagamoyo na kuifanya kuwa mji wa uwekezaji.
“Taratibu
za kuwalipa wananchi ili kupisha eneo la kilomita 100 za mraba
zimekamilika na ndani ya mwaka huu mchakato huo utahitimishwa kabla
wawekezaji hawajaanza kukaribishwa,” alisema.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa EPZ, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia alisema
Serikali imeuagiza kila mkoa kutenga eneo la uwekezaji ili kuongeza
idadi ya viwanda vilivyopo nchini.
“Kwa sasa EPZ zinaingiza kiasi cha dola bilioni moja za Marekani (zaidi ya Sh2 trilioni) kwa mwaka.Serikali
kwa kushirikiana na Singapore imetenga dola 10 bilioni (zaidi ya Sh20
trilioni) ambazo zitatumika kujenga mji wa Bagamoyo,” alisema Kanali
Simbakalia.
Mikoa mingine iliyotengwa kwa ajili ya kujenga EPZ ni Kigoma, Morogoro na Mtwara.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Mhe. Charles Mwijage akimtambulishaMkurugenzi
Mkuu wa EPZA, Mhe. Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia
Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mwijage akimwelezea Rais wa
Vietnam, Mhe. Truong shughuli zinazofanywa na Kampuni ya Simu ya Halotel
kutoka nchini Vietnam, ambapo alimwonyesha Vocha za muda wa maongezi za
mtandao huo ambazo zinapatikana katika gharama tofauti kulingana na
nafasi ya kifedha ya mtumiaji.
Mhe.
Mwijage akiwasilisha taarifa ya Wizara juu ya fursa za uwekezaji
zilizopo nchini Tanzania, hali halisi ya uwekezaji katika kituo cha EPZA
na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuanzisha maeneo ya
uwekezaji katika mikoa yote nchini kufuatia shughuli za kiuchumi
zinazofaa katika Mkoa husika.
0 comments:
Post a Comment